Sh mil 500 kuboresha tiba kwa wananchi 72,000 Musoma

AWAMU ya kwanza ya ujenzi wa kupandisha hadhi zahanati ya Rwamlimi katika Manispaa ya Musoma mkoani Mara kiwe kituo cha afya umekamilika kwa asilimia 95.

Mganga Mfawidhi wa Zahanati hiyo, Dk Aisha Shaban alilieleza HabariLEO kuwa mradi huo wenye thamani ya Sh milioni 500 zilizotolewa na serikali kuu ulianza kutekelezwa Desemba 12 mwaka jana baada ya kupokea Sh milioni 250.

Dk Shaban alisema hatua ya kwanza inahusu ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na eneo la kuchomea takataka na kwamba wanachimba na kujengea mashimo ya vyoo (makaro) mawili makubwa na chemba 40.

Dk Shaban alisema Aprili 19 mwaka huu walipokea Sh milioni 250 nyingine kwa ajili ya hatua ya pili ya ujenzi wa majengo ya mama na mtoto, upasuaji, jengo la kufulia na kupigia pasi ambayo mpaka wakati akizungumza yalikuwa yamekamilishwa kwa asilimia 50.

Dk Shaban alisema mradi umetoa ajira za muda mfupi zaidi ya 100 kwa watu wa kada tofauti wakiwamo wa ndani ya kata hiyo.

Alisema kituo hicho cha afya kitahudumia watu zaidi ya 72,000 kutoka kata za Rwamlimi, Mshikamano, Nyakato na Kwangwa.

Dk Shaban alisema kituo hicho kitakuwa na vitanda vinne vya kujifungulia kwa wakati mmoja na wodi tatu zitakazohudumia wazazi 30 kwa pamoja, hivyo kupunguza msongamano wa jawazito kwenye Kituo cha Afya Nyasho.

Alisema Jengo la OPD lina vyumba viwili vya madaktari, chumba cha kuuzia dawa, wodi mbili za mapumziko (wanawake na wanaume), eneo la kufanyia upasuaji mdogo, chumba cha kutibia vidonda, chumba cha sindanoo, mapokezi na sehemu ya malipo.

Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inaeleza kuwa chama hicho kitaendeleza jitihada kwa kutoa kipaumbele katika sekta ya afya kwa kuwa inagusa maisha ya Watanzania na ustawi wa taifa, ili wananchi wawe na afya, siha bora.

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 ambao ni mwendelezo wa jitihada za kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 pamoja na mengine unaahidi kuboresha hali ya maisha ya Watanzania wote.

Serikali inatekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya afya kuanzia ngazi ya jamii hadi mkoa kwa ajili ya kutoa huduma za tiba, bobezi na kibingwa ili kuhakikisha akinamama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano wanapata huduma bora za tiba.

Habari Zifananazo

Back to top button