Sh milioni 30 kusaidia elimu wasichana jamii ya wafugaji

ZAIDI ya Sh milioni 30 zimechangwa na Shirika la Mipango na Maendeleo ya jamii Longido (CBO) na Shirika mwenza la nchini Marekani la Friends For African Development (FAD) kwa kushirikiana na wananchi na Mbunge wa Jimbo la Longido mkoani Arusha, Dk Steven kiruswa Katika kuhakikisha mtoto wa kike wa jamii ya kifugaji anapata elimu ya uhakika na huduma za kijamii.

Hayo yalisemwa na  Dk Kiruswa katika kitongoji cha Kale, kijiji cha Iloirienito kata ya Iloirienito wilayani humo mara baada ya kushiriki tukio la nguvu kazi na wananchi baada ya kuona juhudi  za wananchi katika kuisaidia serikali ujenzi wa madarasa mawili kwa kuzomba Mawe, kulipa gharama za mchanga na kumlipa fundi zimemvutia yeye binafsi na marafiki zake kutoka nchini Marekani kusaidia zaidi ya Dola 10,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na uvutaji wa maji kutoka katika chanzo cha maji kilichopo Mlimani.

Kiruswa ambaye pia ni Naibu Waziri wa Madini alisema kuwa juhudi hizo zimempa nguvu yeye kuchangia matofali 1000 ,sementi mifuko 100,mbao na gharama nyingine kwani shule hiyo bado haijasajili na juhudi zaidi zinahitajika ili ifikapo januari shule hiyo iweze kusajili rasmi na serikali kwa manufaa ya wakazi wa eneo hilo ambao kwa kiasi kikubwa wana kiu ya elimu baada ya kuifuta umbali mrefu kwa miaka mingi.

Alisema kuwa awali wanafunzi wa shule hiyo walikuwa wakitembee umbali wa zaidi ya km 16 kwenda na kurudi shule lakini baada ya ujenzi wa madarasa kwa ushirikiano wa mashirika hayo,Mbunge na wananchi yameongeza jitihada zaidi kwa wananchi kupeleka watoto shule kwa kuwa huduma hiyo ya elimu kwa sasa imewafikia karibu.

Akizungumzia maji,Kiruswa alisema kuwa FAD ilituma zaidi ya dola 10,000 kwa ajili ya kuvuta maji kutoka katika vyanzo vya maji vilivyoko mlimani na kwenda Kijijini baada ya kuona kuna changamoto kubwa ya maji katika Kijiji cha Iloirienito.

Kiruswa alisema Shirika hilo la Marekani limekuja kuangalia kama fedha zilizotumwa kwa ajili ya miradi hiyo zimefanya kazi na baada ya kujionea wenye jitihada za miradi hiyo kufikia hatua nzuri wameridhishwa na kuahidi kutoa msaada tena kwa ajili ya Kijiji hicho na Longido kwa ujumla.

’’Hizi jitihada zinatakiwa kupongezwa na zinawapa nguvu wafadhili kuendelea kusaidia Jimbo la Longido hivyo nasi tunapaswa kuongeza jitihada ili shule hii iweze kusajili ifikapo januari mwakani’’alisema Mbunge

Rais wa FAD,Professa Benson Fraser na Makamu wake Justin Caplan wamefurahishwa na uwajibikaji wa wananchi wa Kijiji cha Iloirienito kwa jinsi wanavyojituma katika kuisadia serikali kwa ajili ya elimu na maji na kusema kuwa dola wanazotuma zimefika katika mikono salama.

Wamarekani hao walisema kuwa FAD itaendelea kuisaidia jamii ya kifugaji ya Kimasai ya wilayani Longido kwa kuwa wameonyesha uamianifu na kujituma kwa ajili ya watoto wa kike na kiume katika suala la elimu.

Naye Diwani wa kata ya Iloirienito,Sano Oltus alimshukuru Mbunge wa jimbo la Longido na FAD kwa jinsi wanavyojitoa katika shughuli za maendeleo na kusema kuwa yeye kwa kushirikiana na viongozi wa serikali ngazi ya kitongoji na Kijiji watahakikisha wanajitoa ili kulinda heshima wanayopewa.

Habari Zifananazo

Back to top button