Sh milioni 78 kuchangia masuala ya lishe Msalala

HALMASHAURI ya Wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga imetenga bajeti ya zaidi ya Sh milioni 78 kwa ajili ya kuchangia shughuli mbalimbali za lishe, huku wakina mama wakitakiwa kuzingatia makundi 6 ya vyakula ili watoto waweze kupata afya bora.

Kauli hiyo imetolewa Novemba Mosi 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Rose Manumba wakati akizungumza na wakina mama wa Kata ya Segese katika maadhimisho ya Siku ya Lishe Duniani.

Advertisement

Manumba amesema kushiba pekee sio lishe bora bali wanatakiwa kuzingatia namna sahihi ya uandaaji wa chakula kwa kuzingatia makundi yote ya vyakula.

“Wakina mama hakikisheni mnazingatia lishe bora kwa watoto wenu kwa kuzingatia makundi sita ya lishe ili kuondokana na magonjwa na hali ya udumavu’’ amesema Manumba.

Ofisa Lishe Halmashauri ya Msalala Peter Nganzo ametoa mafunzo juu ya uandaaji wa chakula bora kilicho zingatia makundi yote ya chakula ili watoto waweze kuwa na lishe bora itakayo wasaidia katika makuzi yao na kutokupata magonjwa yanayotokana na ukosefu wa lishe bora.

Ngazo amesema Katika maadhimisho hayo ya lishe yamehudhuriwa na wataalumu mbalimbali kutoka katika Halmashauri hiyo pamoja na wananchi wa Kata ya Segese.