Shahidi aeleza alivyokuta mifupa kesi ya polisi Mtwara

MTWARA; SHAHIDI Ahobokile Mwandiga wa kitengo cha uchunguzi wa kisayansi wa Jeshi la Polisi katika kesi ya mauaji inayowakabili maofisa saba wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara, ameieleza mahakama kuwa alipofika eneo linalodaiwa la mauaji alishuhudia mifupa minane ambayo ni mbavu.
Maofisa hao wa jeshi hilo la Polisi mkoani hapa wamefikishwa mahakamani hapo kwa tuhuma za kufanya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamisi (25) Mkazi wa Kijiji cha Ruponda wilayani Nachingwea mkoani Lindi.
Shahidi huyo alidai mbele ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara chini ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Hamidu Mwanga kuwa Januari 22, 2022 majira ya saa 2:00 asubuhi akiwa katika ofisi za jeshi hilo aliitwa na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO) kumjulisha kuhusu kupotea kwa mfanyabiashara huyo.
Hivyo alijiandaa kwa kubeba vifaa vyake vya kazi, ikiwemo kamera kisha kutakiwa kuelekea eneo lililohisiwa kutupwa mwili wa mfanyabiashara huyo anayedaiwa kuuawa na maofisa hao.
“Tuliondoka kituoni kuelekea eneo la tukio huko Hiari tukiwa tumeongozana na RCO pamoja na maaskari wengine na huko tuliwakuta watu wengine ambao RCO aliwapigia simu waje eneo hilo, akiwemo daktari kutoka Hospitali ya Rufaa ya Ligula na Mkemia Mkuu wa Serikali, tulipoanza kutafuta tukaanza kuona mifupa minane iliyodhaniwa kuwa ni mbavu,” alidai shahidi huyo.
Alisimulia: “Tulipoendelea kutafuta tukaona suruali yenye rangi ya buluu, pia tukaona eneo lenye mkusanyiko wa funza kisha mifupa mingine miwili inayodhaniwa kuwa ni miguu baada ya hapo nikaviwekea alama kila kimoja na kisha kuvifunga kwenye bahasha kwa kushirikiana na mkemia wa serikali na baadaye nikavipiga picha”.
Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la mawakili 17, wakiwemo tisa kutoka upande wa Jamhuri na wanane upande wa utetezi ambapo ilihamishwa kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo.
Mauaji hayo yalifanyika baada ya mfanyabiashara huyo kudai fedha zake Sh 33,748,980 ambazo maofisa hao wa Jeshi la Polisi wanadaiwa kuzichukua kutoka kwake wakati walipomfanyia upekuzi.
Washitakiwa hao akiwemo Mrakibu wa Polisi, Gilbert Kalanje ambaye ni Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Mtwara, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Charles Onyango ambaye ni Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara, Mrakibu wa Polisi Msaidizi, Nicholaus Kisinza ambaye ni Mkuu wa Kikosi cha Intelejensia ya Jinai Mkoa wa Mtwara.
Wengine ni Mkaguzi wa Polisi, John Msuya Mganga, Mkuu wa Zahanati ya Polisi mkoani Mtwara, Mkaguzi wa Polisi Msaidizi Marco Mbuta, Mkaguzi wa Polisi Shirazi Mkupa pamoja na Koplo Salimu Mbalu.
Mauaji hayo yalifanyika Januari 5, 2022 huku mwili wa mfanyabiashara huyo ukikutwa umetupwa katika Kitongaji cha Majengo, Kijiji cha Hiari, Wilaya ya Mtwara.



