Samia: Tutaendelea kulinda amani

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania itaendelea kulinda amani, umoja wa kitaifa na utulivu wa kisiasa.

Alisema hayo alipopokea salamu za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), António Guterres zilizowasilishwa kwake na Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa UN, Parfait Onanga-Anyanga, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma jana na akasema utulivu kisiasa umekuwa msingi wa maendeleo ya nchi.

Rais Samia alisema Tanzania itaendelea kushirikiana na UN na jumuiya za kimataifa katika kukuza demokrasia, utawala bora na maendeleo jumuishi.

Alituma salamu za shukrani na kupongeza hatua ya Guterres kutuma ujumbe maalumu nchini Tanzania ili kupata uelewa kuhusu hali ya nchi na kusikiliza maoni ya wadau.

Rais Samia alisema serikali ya Tanzania imejizatiti kuhakikisha mchakato wa kufuatilia matukio ya uvunjifu wa amani ya kabla na wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, mwaka jana unafanyika kwa kuzingatia misingi ya utawala wa sheria, uwajibikaji na haki.

Aidha, alisema serikali iko tayari kupokea na kuyafanyia kazi mapendekezo yatakayowasilishwa na Tume ya Uchunguzi baada ya kukamilika kwa kazi yake.

Rais Samia alisema mapendekezo hayo yatakuwa sehemu muhimu ya mchakato wa kuimarisha maridhiano ya kitaifa na marekebisho ya katiba.

Onanga-Anyanga yupo nchini Tanzania kusikiliza maoni ya wadau na kutathmini hatua zinazochukuliwa na serikali katika kuimarisha utulivu wa kisiasa, mshikamano wa kitaifa na kuendeleza misingi ya utawala wa sheria kufuatia matukio ya uvunjifu wa amani ya kabla na wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, mwaka jana.

Alisema UN inatambua na kupongeza hatua zinazochukuliwa na serikali ya Tanzania baada ya matukio hayo, hususani uamuzi wa kuunda Tume Huru ya Uchunguzi na dhamira ya kufanya mazungumzo jumuishi ya kitaifa na kuendeleza mchakato wa mabadiliko ya kikatiba.

Aliongeza kuwa UN inaendelea kuitambua Tanzania kama nchi yenye historia ya muda mrefu ya amani, utulivu wa kisiasa na mshikamano wa kitaifa na kuthamini mchango wake katika juhudi za kulinda na kuimarisha amani Afrika.

Onanga-Anyanga alikutana na kuzungumza na viongozi wa taasisi nchini, ikiwemo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahakama ya Tanzania, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa pamoja na viongozi wa vyama vya siasa.

Aidha, alikutana na kuzungumza na mwenyekiti na wajumbe wa Tume Huru ya Uchunguzi na wadau wengine wa kisiasa na kijamii ili kupata maoni na mitazamo tofauti kuhusu masuala yaliyotokea na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na serikali.

Onanga-Anyanga alisema mashauriano hayo yataiwezesha UN kupata taswira halisi kuhusu uhalisia wa matukio ya Oktoba 29, 2025 na juhudi zinazofanywa na serikali ya Tanzania katika utatuzi wa changamoto zilizojitokeza wakati na baada ya matukio hayo.

Alisema hatua hizo zina mchango muhimu katika kuimarisha maridhiano ya kitaifa, kurejesha imani ya wananchi na kuendelea kujenga taasisi imara za kidemokrasia nchini

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button