Shehe Alhad akabidhi ofisi, ataja vishindo Bakwata

ALIYEKUWA Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Salum amekabidhi ofisi rasmi kwa Kaimu Shehe, Walid Alhad Omar na kumshauri kuwa mvumilivu kwani ndani ya Baraza Kuu la Waislamu (Bakwata) kuna vishindo vingi.

Amesema yuko tayari kumpa ushirikiano mrithi wake kwa kuwa amekuwa na uzoefu kwa miaka mingi, na anaamini pia kiongozi huyo ni mzoefu na anaweza kuisaidia Dar es Salaam.

Shehe Alhad alisema hayo jana Dar es Salaam baada ya kukabidhi ofisi kwa Shehe Walid na kusisitiza kuwapo ushirikiano na umoja ndani ya Bakwata na kwamba Mungu ndiye anapanga akitakacho.

Hivi karibuni, Bakwata Taifa kupitia Baraza la Ulamaa lilitengua uteuzi wa Shehe Alhad na kumteua Shehe Walid Omar kukaimu nafasi hiyo.

Shehe Alhad alishauri kuendelea kulisaidia baraza akishirikiana na chombo hicho kwani yeye ni mtoto wa baraza akiwa ameishi na analijua vizuri, na mpaka sasa ni Katibu wa Kamati ya Mwezi Bakwata Taifa hivyo ataendelea kulitumikia kwa nafasi hiyo au yoyote.

“Nitaendelea kuwa ndani ya baraza kulitumia kwa nafasi yoyote. Ndani ya baraza wanaofanya kazi sio malaika wana mapungufu ambayo tumekuwa tukivumiliana hivyo tumuombee Shehe Walid katika nafasi hiyo,” alisema.

Aliongeza: “Umoja wetu ndani ya baraza ni kitu kikubwa, baraza likipata doa au kupasuka athari kubwa kwa Waislamu, kitu ambacho hatutarajii kitokee, tuwe wamoja tuisaidie serikali yetu na tumuuunge mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake.”

Aidha, alisema akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano Tanzania, atashirikiana na Shehe Walid kufanya kazi pamoja akiwa kama mwasisi wa kamati za amani Tanzania zinazosaidia taifa kwa ujumla.

Alisema uteuzi wa Shehe Walid ni sahihi, mwenye uwezo na ni marafiki, hivyo wanaojaribu kuwaweka mbali hawataweza bali wataendelea kuimarisha Bakwata.

“Nikukaribishe, kuna vishindo vingi, vumilia jenga baraza, mengi yatakukuta…vumilia tutasaidiana na Waislamu wa Dar es Salaam kulivusha baraza,” alisema Shehe Alhad na anamwomba Mungu ambariki.

Naye Shehe Walid alisema mtu ni maneno na vitendo, na kinachopimwa ni vitendo hivyo anamshukuru Mungu kwa kuwa yeye ameyapanga.

Alisema anayempisha ni shehe na aliyeingia ni shehe na lililotokea ni jambo la kawaida kwani kazi yao lengo lake moja ni kufanya kazi ya Mungu.

 

Habari Zifananazo

Back to top button