Sheria, kanuni vyataja masharti uteuzi kugombea urais uchaguzi

SHERIA ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Namba 1 ya mwaka 2024 inataka mgombea wa kiti cha rais awasilishe fomu za uteuzi si zaidi ya saa 10 kamili alasiri siku ya uteuzi.

Kwa mujibu wa sheria hiyo fomu hiyo inatakiwa iwe na jina, jinsi, hali ya ulemavu, ikiwa ipo na anwani ya mgombea wa kiti cha rais na cha Makamu wa Rais ambaye atakuwa ni mgombea mwenza.

Sheria pia inataka fomu hiyo iwe na tamko la mgombea kwamba yupo tayari na ana sifa za kuwa mgombea katika uchaguzi.

Fomu hiyo pia inatakiwa iwe na kiapo cha mgombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano kitakachojazwa na kusainiwa mbele ya jaji.

Sheria inataka fomu hiyo iwe na majina na anwani za wadhamini, namba za kadi za kupigia kura za wadhamini na uthibitisho wa msimamizi wa uchaguzi kuhusu wadhamini kutoka katika jimbo husika.

Kanuni za uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani zinataka mgombea anayependekezwa kwa ajili ya uchaguzi  wa rais, kabla ya saa kumi alasiri siku ya uteuzi atawasilisha kwa tume fomu yake ya uteuzi yenye jina,

Jinsi, hali ya ulemavu, ikiwa ipo na anwani ya mgombea wa kiti cha rais na cha makamu wa rais ambaye atakuwa ni mgombea mwenza.

Kanuni pia zinataka fomu hiyo iwe na tamko la mgombea kwamba yupo tayari na ana sifa za kuwa mgombea katika uchaguzi na kiapo cha mgombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano kitakachojazwa na kusainiwa mbele ya jaji.

Kanuni pia zinataka fomu iwe na majina na anwani za wadhamini, namba za kadi za kupigia kura za wadhamini na uthibitisho wa msimamizi wa uchaguzi kuhusu wadhamini kutoka katika jimbo husika.

Kanuni zinaeleza endapo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) itaridhika kuwa mgombea wa kiti cha rais na makamu wa rais anayependekezwa ana sifa za kugombea itathibitisha uteuzi wa mgombea katika Fomu Na. 8A iliyoainishwa katika Jedwali la Kwanza.

Pingamizi
Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani zinaeleza pingamizi dhidi ya uteuzi wa mgombea wa kiti cha rais na makamu wa rais linaweza kuwekwa na mgombea mwingine, Msajili wa Vyama vya Siasa au Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kwa mujibu wa kanuni hizo pingamizi litakalowekwa na Msajili wa Vyama vya Siasa litajikita katika masharti ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi pekee.

Kanuni zinaeleza kwa kuzingatia masharti ya kanuni ndogo ya (1)- (a) mgombea au Mwanasheria Mkuu wa Serikali atawasilisha pingamizi kwa Tume si zaidi ya saa 10 kamili alasiri ya siku inayofuatia siku ya uteuzi.

“Msajili wa Vyama vya Siasa atawasilishwa pingamizi kwa Tume ndani ya siku kumi na nne baada ya siku ya uteuzi,” zinaeleza kanuni.

Zinaeleza pingamizi dhidi ya uteuzi wa mgombea wa kiti cha rais na makamu wa rais litawasilishwa kwa Tume kupitia Fomu Na. 9A iliyoainishwa katika Jedwali la Kwanza.

Kanuni zinataka fomu hiyo iwe na taarifa za mweka pingamizi; taarifa za mgombea anayewekewa pingamizi; sababu za pingamizi, tarehe na muda wa kuwasilisha pingamizi na saini ya mweka pingamizi.

“Endapo Tume itakubali pingamizi dhidi ya uteuzi wa mgombea itafuta jina la mgombea huyo katika orodha
ya wagombea walioteuliwa,” zinaeleza kanuni.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button