Sheria za China Kutambua Kiswahili

DAR-ES-SALAAM : LUGHA ya Kiswahili imetambuliwa rasmi kuwa nyenzo muhimu katika kukuza uelewa wa kisheria na kitamaduni kati ya Tanzania na China, kufuatia uzinduzi wa tafsiri ya kwanza ya maandiko ya kisheria kutoka China kwenda Kiswahili.
Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam katika kongamano lililowakutanisha wataalamu wa tafsiri, wachapishaji na wasomi kutoka nchi hizo mbili, ambapo viongozi wa taasisi mbalimbali waliipongeza hatua hiyo wakieleza kuwa ni mwanzo wa ushirikiano mpya na wenye tija kwa wananchi wa pande zote mbili.
Akizungumza katika kongamano hilo, Prof. Aldin Mutembei, Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, alisema hatua hiyo imefungua milango ya maarifa kwa Watanzania. “Kwa mara ya kwanza, watanzania wataweza kupata maarifa ya sheria za China kupitia lugha wanayoielewa. Hili ni jambo kubwa kwani linarahisisha mawasiliano ya kisheria baina ya nchi hizi mbili,” alisema Prof. Mutembei.
Kwa upande wake, Kulwa Kindija kutoka Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) amesema hatua hiyo inaunga mkono juhudi za serikali kukuza matumizi ya Kiswahili katika sekta ya sheria, huku akieleza kuwa istilahi maalumu zimeanza kuandaliwa ili kurahisisha tafsiri sahihi ya maandiko ya kisheria.
Husna Sharif kutoka Chama cha Maendeleo ya Urafiki kati ya Tanzania na China amesema tafsiri hizo zitasaidia kupunguza migogoro midogo inayotokana na kutokuelewana, hasa katika biashara na uhamiaji. “Kwa lugha ya pamoja, kila upande utaelewa haki na wajibu wake kisheria,” alisema.
Kutoka China, Prof. Ao Manyun wa Chuo Kikuu cha Mawasiliano amesema Kiswahili ni lugha ya kimataifa ambayo imekuwa ikifundishwa nchini humo kwa zaidi ya miaka 65 na zaidi ya wahitimu 540 tayari wamejifunza lugha hiyo.
“Tafsiri ya maandiko ya kisheria ni hatua muhimu katika kuimarisha mahusiano ya kiutamaduni na kisheria. Niliona ni vyema kutafsiri vitabu vya sheria kwa Kiswahili ili kuwasaidia raia wa China wanaofanya biashara Tanzania kuelewa sheria za ndani,” alisema Prof. Ao.
Aliongeza kuwa tafsiri ya sheria, ikiwemo zinazohusu haki halisi, itasaidia wageni kuelewa namna ya kumiliki mali au kushiriki miradi ya pamoja kwa mujibu wa sheria. SOMA: Uamuzi wangu kujifunza Kiswahili umezaa matunda’
Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni ishara ya uhusiano wa kina na wa kimkakati kati ya Tanzania na China, unaojengwa si tu katika misingi ya biashara, bali pia kwa uelewano wa kijamii na kisheria kupitia Kiswahili kama daraja la mawasiliano.




