VIONGOZI, walimu na madaktari wa michezo kutoka Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) wametakiwa kutenda haki na kujiepusha na rushwa za aina yeyote katika michezo ili wasiue vipaji nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego ametoa rai hiyo wakati akifungua mafunzo maalumu yaliyoandaliwa kwa ajili yao kuwakumbusha maadili na sheria mbalimbali zinazosimamia michezo nchini.
Mashindano haya ya SHIMIWI yanatarajiwa kufanyika katika uwanja wa Samora mjini Iringa mwanzoni mwa mwezi yakihusisha wanamichezo zaidi ya 3000 kutoka klabu zaidi ya 70 zinazoundwa na watumishi wa serikali kutoka wizara mbalimbali, idara zinazojitegemea na wakala wa serikali na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.
“Tunapoenda katika michezo tukumbuke michezo ni burudani pia ni ajira kwa vijana wengi hivyo mkatende haki, mjiepushe na msikubali rushwa ya aina yeyote kwani mkifanya hivyo mtaleta chuki, huzuni lakini pia mtawafanya wachukie michezo na hatimaye kuua vipaji. Tunataka Mshindi apatikane kwa haki na atakayeshindwa ajiandae mashindano yajayo aje ashinde kwa haki,” alisema Dendego.
Alisema serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ipo mstari wa mbele kuhakikisha sera ya michezo na michezo inatekelezwa na kuibia vipaji vipya ili kuitangaza Tanzania katika duru za Kimataifa.
“Hamasa aliyoitoa Mheshimiwa Rais katika vilabu vya Simba na Yanga katika mashindano ya kimataifa ilikuwa ni dhamira ya dhati kuitambua na kuipa thamani sekta ya michezo katika nchi yetu,” alisema.
Kwa niaba ya serikali alisema wamejipanga kuupokea ugeni huo mkubwa na kuwahakikishia ushiriano na usalama wa kutosha kwa kipindi chote cha wiki mbili ambacho wanamichezo hao watakuwepo na akahadi upatikanaji wa huduma bora na za uhakika za chakula, malazi na burudani za aina zote.
Awali akitoa taarifa mbele ya Mkuu huyo wa Mkoa, Makamu Mwenyekiti wa SHIMIWI Taifa, Itika Mwankenja alisema mashindano hayo ya wanaume na wanawake yatahusisha mpira wa miguu kwa wanaume, mpira wa pete, kuvuta kamba, riadha, mbio za baiskeli, drafti, bao na karata.
Mbali na hayo aliwaomba Viongozi, wafanyabiashara na wenyeji wa Iringa kutumia fursa ya ujio huo wa wageni kwa kutoa huduma ya usalama, kuuza bidhaa, chakula cha asili ya Iringa (Kihehe), kuandaa huduma za malazi ya bei rafiki na kutangaza fursa zilizopo kwa wageni.
“Kwakuwa kusanyiko hili ni kubwa tunaomba wafanyabiara wajiandae kutupokea sisi kama wageni wao, tunatumai kwa kipindi chote cha wiki mbili tutachokuwa hapa huduma zote za msingi tutazipata msitumie fursa hii kupandisha gharama za bidhaa,” alisema