Shindano mkali wa futari kutoa mpikaji futari bora

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema wilaya yake itakuwa miongoni mwa wilaya nne zitakazoshiriki shindano la “Mkali wa Futari Jikoni na Nishati Safi,” litakalofanyika mwezi huu wa Ramadhani
Hatua hiyo inalenga kuhamasisha wanawake kuongeza thamani ya biashara zao, ikiwemo kununua majiko bora na kuimarisha maeneo ya biashara.
Mpogolo aliyasema hayo leo katika uzinduzi wa msimu mpya wa Kampeni ya Mwanamke Fundi 2025, uliofanyika Dar es Salaam chini ya Africa Media Group Limited (AMGL), ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Amesema kuwa Rais Samia amewahamasisha wanawake katika shughuli mbalimbali, akiwemo kupika futari kwa ustadi mkubwa, huku akifanya kazi zake za uongozi kama Rais wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi.
Mpogolo amesema kuwa Rais Samia ni mfano wa kipekee na kwa sasa tuzo yake haiwezi kuchukuliwa na mtu mwingine yeyote. “Rais Samia ndiye mwanamke fundi namba moja, kampeni hii sasa inatafuta fundi wa pili,” amesema.
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Dk. Gladness Selema, amesisitiza umuhimu wa ufundi wa mwanamke, akisema kuwa ufundi huu unaanzia ndani ya mwanamke kupitia shughuli anazozifanya, na kumtaka kila mwanamke kuwa fundi sio tu jikoni bali pia katika jamii kwa ujumla, akiwemo kulea watoto na kubadilisha jamii.
Mkurugenzi Mtendaji wa Africa Media Group Limited (AMGL), Shaaban Kissu, amezungumzia hatua kubwa zilizopigwa katika kuleta usawa wa kijinsia nchini Tanzania, akisema kuwa licha ya mifumo dume, wanawake sasa wanashiriki katika shughuli za kiuchumi na kuwa na nafasi katika kampuni na biashara.
Kampeni ya “Mwanamke Fundi: Mkali wa Futari Jikoni na Nishati Safi” ni sehemu ya juhudi za Rais Samia katika kukuza usawa wa kijinsia na kuunga mkono masuala ya nishati barani Afrika.



