Shirika la ndege Ubelgiji lasitisha safari zake DRC

SHIRIKA la Ndege la Brussels la nchini Ubelgiji limetangaza kusitisha safari zake za kwenda na kutoka jijini Kinshasa nchini Jamuhuri ya kidemokrasi ya Congo kutokana na machafuko yanayoendelea kwenye eneo hilo.
Uharibifu wa mali umeripotiwa kutokea Kinshasa wakati wa maandamano yalioongozwa na raia wenye hasira kutokana na kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama mashariki mwa DRC, yaliyosababisha pia uvamizi katika Balozi za Kenya, Uganda, Rwanda, Ufaransa, Marekani na Ubelgiji.
Tayari mataifa ya Ufaransa, Kenya pamoja na Umoja wa Ulaya yamelaani vikali uvamizi uliotokea kwenye balozi zake.
Shirika hilo limesema litatangaza wakati wa kurejea tena kwa safari hizo baada ya kuangalia na kujiridhisha kwa umakini kuhusu hali ya usalama. Shirika hilo huwa na safari za kila siku kutoka Brussels hadi Kinshasa na kurejea kwenda Brussels.



