SHIRIKA la Changamoto za Mileniala Serikali ya Marekani (Millennium Challenge Corporation-MCC) limeridhishwa na mageuzi ya mifumo ya kiutendaji, yaliyofanywa na Serikali ya Tanzania katika maeneo mbalimbali ikiwemo uimarishwaji wa demokrasia, utawala bora na haki za binadamu.
Sifa hizo zimetolewa leo Oktoba 18 na Mkurugenzi wa Sera na Tathmini wa Shirika hilo, Dan Barnes na kuongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya serikali, wameridhishwa na hatua mbalimbali zilizochangia kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi nchini.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Barnes amesema Bunge la Marekani limeridhia Tanzania kuendelea kunufaika na ufadhili wa shirika hilo la MCC, baada ya kuridhishwa na utendaji wa serikali.
Maamuzi hayo yataifaya Tanzania kuendelea kupewa misaada katika shughuli za maendeleo ambazo zitasaidia kuinua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahamoud Thabit Kombo akizungumza katika mkutano huo ameeleza Tanzania itaendelea kuheshimu na kuenzi uhusiano mzuri uliopo kati yake na Marekani uliodumu kwa zaidi ya miongo sita, huku zikishirikiana katika sekta mbalimbali.
Aidha, Waziri Kombo alisisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuheshimu na kutekeleza misingi ya demokrasia na utawala bora na haki za binadamu ambazo ni tunu za nchi hizo mbili.