Shirika lawakumbuka watoto wenye uhitaji Krismas

SHIRIKA la maendeleo ya vijana linalopambana na maambukizi ya HIV (YAAPA) limetoa misaada mbalimbali ya vyakula kwa watoto wenye mahitaji wanaosomeshwa na shirika hilo katika masomo ya awali (chekechea) kwa ajili ya Krismas.

Mratibu wa shirika hilo, Alex Luoga amekabidhi misaada hiyo kwa watoto hao ikiwa ni kuendana na mpango wa shirika hilo kusaidia jamii katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu na stadi za maisha.

Luoga alisema watoto waliopata misaada hiyo wanatokana na watoto kutoka familia zisizo na uwezo ambao wanahudhuria masomo ya awali kwenye kituo cha shirika hilo sambamba na watoto wanaoishi kuzunguka kituo hicho ambao wametambuliwa na mamlaka za serikali za mitaa.

Aliitaja zawadi zilizotolewa kwa watoto hao kuwa ni pamoja na mchele, unga wa ngano, maharage, biskuti na juice na fedha za kufanikisha hilo zinatokana na sehemu ya ada kidogo zinazotolewa na wazazi wa watoto hao na msaada kutoka Church of Christ True Eternal Light and Love.

Akizungumzia misaada hiyo mmoja wa viongozi wa kanisa hilo, Kabwe Litungi alisema kuwa kanisa hilo linashirikiana na shirika hilo katika kusaidia jamii kila uwezo unaporuhusu kufanya hivyo kama ambavyo wamefanikiwa kusaidia misaada hiyo ya chakula kwa watoto hao.

Baadhi ya watoto hao akiwemo Monica Isack wameshukuru kwa msaada na zawadi hizo kwani zimewafanya kuona kama wao pia wanao watu ambao wanawajali kutokana na  mazingira waliyonayo.

Habari Zifananazo

Back to top button