Shule Rufiji yakabiliwa na changamoto ya vitabu

SHULE ya Sekondari ya Wasichana ya Samia, iliyopo Kata ya Mgomba iliyopo Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, inakabiliwa na changamoto ya vitabu hali inayotishia ufauluwa wanafunzi waliopo.

Hayo yamebainika katika ziara ya Kamati ya Huduma za Kijamii kutoka Shehia ya Kizimkazi Dimbani Zanzibar ilipotembelea wilaya hiyo kujifunza na kujionea miradi ya miundombinu iliyotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii ( TASAF).

Akizungumza mbele ya kamati hiyo ambayo ilifika katika shule hiyo, Mwanafunzi Shaima Ponela ameeelezea changamoto hiyo na ya maji wanayoyatumia kuwa yana chumvi nyingi hayafai kunywa wala kuogea.

“Pamoja na changamoto hizi tunaishukuru sana Serikali kwa nafasi ya kuwezesha shule hiyo kujengwa. Kwa sisi tuliopata nafasi ya kuwepo katika shule hii, tunaahidi kusoma kwa bidii ili kuleta heshima kwa Rais wetu kama jina la shule lilivyo.” amesema.

Akizungumza kwa niaba ya wazazi ambao wanafunzi wanasoma katika shule hiyo, John Maselle ameipongeza serikali kwa kuona changamoto iliyokuwa inawakabili watoto wao kwa kujenga shule hiyo japokuwa bado ina changamoto.

” Shule hii bado ina upungufu wa vitabu, maabara, pia tunaomba walimu waongezwe,” amesema.

Mkuu wa Shule hiyo, Rose Ushaki amesema wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo ni wale wenye ufaulu wa juu wa alama A, wanasomea mchepuko wa sayansi hivyo jukumu lao kubwa ni kuhakikisha wanaendeleza ufaulu huo.

” Hii ni sekondari mpya ya bweni, tunatarajia tukifungua shuleJulai, tutakuwa na maboresho kwa baadhi ya mambo,” amesema.

Akitoa taarifa ya shule hiyo Mtendaji wa Kijiji cha Mgomba Kati, Flora Magoti amesema Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji ilipokea Sh milioni 149.6 Septemba mwaka jana ikiwa ni fedha kutoka TASAF kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vienne vya madarasa na matundu nane ya vyoo.

Amesema ujenzi huo ulianza kama hitaji la wananchi wa eneo la Mpima Kata ya Mgomba baada ya kuona watoto wanasafiri umbali mrefu.

Naye Mratibu kutoka Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Makame Ally Haji amesema wanaamini sekondari hiyo itakuwa nzuri na itatoa wahitimu ambao baadhi yao watakuwa viongozi wazuri wenye kuleta maendeleo nchini.

Kwa upande wake Mratibu wa Tasaf Wilaya ya Rufiji, Pamella Birukila amesema halmashauri hiyo inatekeleza miradi ya miundombinu katika Kata ya Mgomba na Utete, hivyo sh milioni 361 zimepokelewa kwa ajili ya utekelezaji wake.

” Shilingi milioni 149.6 ni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manne na matundu nane ya choi eneo la Mpima kata ya Mgomba,” amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button