Shule yapania michuano ya vijana Afrika Mashariki

ARUSHA: Shule ya Msingi ya Highridge imesema imejiandaa vyakutosha kuelekea mashindano ya vijana kwa nchi za Afrika Mashariki ‘Chipukizi Cup’ yatakayofanyika Desemba 15 hadi 21 mwaka huu.
Mkurugenzi na kocha wa Highridge, Adam Washokera amesema maandalizi yanaendelea vizuri ikiwemo kuwaandaa vijana wao ili kuwakilisha vizuri taifa.

Amesema wamekuwa na mipango mbalimbali shuleni ukiacha elimu wanayoitoa wameweza pia kuendesha michezo mbalimbali na imeendelea kufanyika ikiwa na lengo la kuibua vipaji kwa vijana ambapo wanafundisha soka na netiboli pia mbio za riadha.
“Tumejikita sana kwenye mpira wa miguu na netiboli na sasa tumefungua Highridge football academy na tumeweza kushiriki mashindano mbalimbali ikiwepo Chipkizi cup 2020 na tukachukua kombe pia 2023 kwa vijana chini ya miaka 9 na tumeshiriki pia Nane nane Cup,” amesema Washokera.
Mashindano ya vijana kwa nchi za Afrika yatafanyika Arusha Desemba mwaka huu yakihusisha zaidi ya timu 330 kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Naye Rehema Washokera amesema hivi sasa wapo katika maonyesho ya 31 ya Nanenane kanda ya Kaskazini kuonyesha vitu ambao wanafanya shuleni hapo na vinavyofanywa na wanafunzi katika masuala mbalimbali ikiwemo ya ubunifu na michezo.
“Katika maonyesho haya tumeleta watoto waonyeshe mambo wanayofanya ambayo ni ujuzi wa ubunifu ambao unaiwezesha akili yake ifanye vitu ambayo vitawasaidia wao kuibua na kutengeneza miradi mbalimbali ikiwemo umwagiliaji,”amesema.



