‘Si majanga yote ya moto majumbani chanzo TANESCO’
Matumizi Mabaya ya Nishati zingine vyatajwa kuongoza kama chanzo cha majanga ya moto nchini

GEITA: KAMANDA wa Jeshi la zima moto na Uokoaji mkoani Geita, Kamanda Mratibu Hamis Dawa amesema kuwa majanga mengi ya moto yanayozuka majumbani hayasababishwi na umeme wa Shirika la Umeme (TANESCO) bali ni matumizi holela ya vyombo vya umeme pamoja na kutochukua tahadhari ya vifaa bora na mkandarasi sahihi aliyehakikiwa kwaajili ya kutandaza nyaya katika nyumba zao.
Kamanda Dawa ameyasema hayo mwishoni mwa juma alipotembelea banda la TANESCO katika Maonesho ya Biashara, Viwanda na Kilimo mkoani Geita.
Amesema kuwa jukumu la TANESCO ni kupeleka umeme kwa mteja mpaka kwenye mita lakini suala la umeme ndani ya nyumba ni suala la mteja kuhakikisha nyaya ndani ya nyumba yake zimetandazwa vizuri, na vifaa vyote vilivyotumika vinaubora ikiwemo saketibreka.
Soma pia: https://habarileo.co.tz/chanzo-umeme-kukatika-usiku-wa-manane/
Akizungumzia matumizi holela ya vyombo vinavyohitaji nishati ya umeme yanayoweza kupelekea majanga ya moto kamanda hayo amefafanua kuwa ni muhimu kwa watumiaji umeme kuhakikisha wanatumia vifaa vya Umeme vyenye ubora kwa umakini na kuzima kila baada ya kutumia vifaa hivyo
“Kuna vifaa vingine vya Umeme vinaweza kujizima vyenyewe baada ya kutumia Umeme kwa kiwango kinachotakiwa (energy efficiency) na vina uwezo wa kudhibiti umeme, vifaa hivyo ni kama Ac na Friji, lakin vifaa kama pasi na jiko,unaposahau kuzima baada ya matumizi vinaweza kuwa chanzo cha moto, na utasema tatizo ni Umeme wa TANESCO lakini chanzo ni matumizi holela yasiyozingatia utaratibu sahihi wa kuvitumia”alisema kamanda hamis dawa
Ameongeza kwa kusema kuwa Katika matumizi ya Nishati safi ya kupikia, Jeshi la Zimamato na uokoaji, limeanza kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya Nishati safi ya kupikia ikiwa ni Nishati ya Umeme na gesi ili kuepusha majanga ya moto.
Kwa upande wake Meneja wa TANESCO Mkoa wa Geita, Mhandisi Joachim Ruweta, amesema kuwa TANESCO mkoani humo inashirikiana kwa ukaribu na Jeshi la Zima Moto na Uokoaji, kwa kufanya kazi kwa kushirikiana kwani kazi zao zinategemeana
“Tunafanya kazi kwa ushirikiano sana na Jeshi la zima moto hapa Mkoani Geita, wanapopokea Taarifa ya moto, wanatupigia na sisi ili twende kuzima Umeme, kwasababu kuna kemikali zingine wanazozitumia , haziendani na Umeme, hivyo wao hawawezi kuzima moto bila kutushirikisha” amesema Mhandisi Joachim.
Soma pia: https://www.tanesco.co.tz/media/view-news-archive?id=72
Akihitimisha, mhandisi huyo Joachim ametoa rai kwa wananchi kutumia vifaa vya Umeme kwa umakini, na kukagua njia za Umeme ndani ya nyumba zao kila baada ya Miaka mitano, ili kuepuka matatizo mbalimbali ya Umeme kama upotevu wa Umeme, na majanga ya moto.