‘Hapana tena ukatili wa kijinsia’

MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Mama Mariam H. Mwinyi, ameendelea kutekeleza kwa vitendo dhamira ya kukomesha ukatili wa kijinsia kupitia kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia inayoendelea nchi nzima.
Kampeni hiyo inalenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia, mbinu za kujilinda, pamoja na kuhamasisha hatua za pamoja katika kukabiliana na tatizo hilo. SOMA: Ukatili wa Kijinsia Unaendelea Kuathiri Jamii

Takwimu za mwaka 2024 zinaonesha ukubwa wa changamoto hiyo, ambapo kesi 1,809 za ukatili wa kijinsia ziliripotiwa nchini, kati yake 1,525 zikiwa zinawahusu watoto. Hali hiyo imeendelea kuibua kilio cha kuimarishwa kwa ulinzi wa watoto na juhudi za pamoja za jamii katika kupambana na vitendo hivyo.
Katika kuendeleza kampeni Mama Mariam alitembelea Vijana wa Makachu pamoja na vikundi vya wanawake wajasiriamali Forodhani, Mkoa wa Mjini Magharibi. Ziara hiyo imeongeza hamasa kwa makundi hayo huku ikisisitiza umuhimu wa mshikamano wa wananchi katika kulinda haki na ustawi wa wanawake na watoto.

Akiwa ameambatana na Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya ZMBF, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo pamoja na watumishi, Mama Mariam alihimiza jamii kuendelea kupaza sauti kupitia ujumbe wa “No More Campaign” kwa kusisitiza kaulimbiu “Hapana Tena kwa Ukatili”.
Kampeni ya Siku 16 inaendelea kuwa jukwaa muhimu la kutoa elimu, kuhamasisha hatua madhubuti na kuimarisha mshikamano wa jamii katika kukomesha ukatili wa kijinsia, huku ikilenga kujenga Zanzibar na Tanzania yenye amani, usawa na ustawi kwa wote.




