Silaa aunda timu kutatua mgogoro sugu wa ardhi Dodoma

DODOMA: Waziri wa Ardhi Nyumba, na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa amemwagiza Katibu Mkuu wizara hiyo kuunda timu ya wataalam kutoka wilaya za mkoa wa Dodoma na mikoa jirani kufanya uhakiki wa umiliki wa ardhi kwa wananchi wa kata ya Mnadani na Nkuhungu jijini Dodoma.

Waziri Silaa ametoa kauli hiyo Februari 15, 2024 jijini Dodoma wakati akihitimisha zoezi la Kliniki ya Ardhi ambayo imekuwa ikiendelea katika kata hiyo.

Kiongozi huyo ameagiza kuundwa kwa tume hiyo mara moja ikiwa ni hatua muhimu ya kutatua migogoro ambayo imedumu kwa muda mrefu ikichagizwa na baadhi ya wananchi kuvamia maeneo ambayo tayari yamemilikishwa.

“Timu zitakuja uwandani kufanya uhakiki, tutafanya uhakiki shamba la kwanza mpaka shamba la 1397, tutafanya uhakiki wa mikataba iliyoingiwa kuangalia uhalali wake, iliingiwa kwa utaratibu gani, tutafanya uhakiki wa michoro ya mipango miji, tutafanya uhakiki wakina nani walikuwepo mwaka 2019, tutafanya uhakiki ni akina nani waliongezeka baada ya muda huo na nani amewaongeza, timu hizi zikimaliza kazi yake tutakutana tena hapa” amesema Waziri Silaa.

Waziri Silaa ametoa wito kwa Watanzania kuwa suala la ardhi ni suala binafsi na kuwaomba wajiepushe na ufuatiliaji wa masuala ya ardhi kupitia vikundi vidogo vidogo na kutengeneza watu wanaojikusanya kwenye vikundi kuwatengenezea mazingira kwamba watasaidia kufuatilia jambo wanalofuatilia kuhusu ardhi na amewahimza kuwa Serikali ndiye msimamizi wa masuala ya ardhi na yanafuatiliwa kwa uadilifu na uaminifu wa hali ya juu.

 

Habari Zifananazo

Back to top button