Simba kujenga studio, uwanja na kuvaa jezi za kimataifa

DAR ES SALAAM – Klabu ya Simba SC imeingia rasmi katika awamu mpya ya mageuzi makubwa ya kiutawala, miundombinu na biashara, kufuatia ushirikiano wake na kampuni ya Jayrutty Investment Company Limited.
Kupitia mkutano wa utambulisho wa mradi wa kimkakati, viongozi wa klabu hiyo wametangaza mikakati kabambe itakayotekelezwa ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo.
Akizungumza mbele ya viongozi wa klabu na wadau wa michezo, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema kuwa miongoni mwa mambo makubwa yatakayotekelezwa ni ujenzi wa ofisi mpya, studio ya kisasa ya media, na kiwanja kipya cha kisasa chenye uwezo wa kubeba mashabiki 10,000 hadi 12,000.
“Moja ya ahadi ni kujenga ofisi mpya, watu wa menejimenti ya Simba muanze kushangilia. Pia tunajengewa ofisi ya media, ni jambo la kupongezwa. Kwa sasa tunaongoza mitandao yote ya kijamii na hapo bado hatujajengewa studio. Kwa studio hii tunakwenda kuwapita hata Al Ahly na Zamalek,” alisema Ahmed Ally.
Kwa upande wake, Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Jayrutty Investment, CPA Joseph Rwegasira, alieleza dhamira ya kampuni hiyo kuifanya Simba kuwa klabu ya kwanza nchini kuvaa jezi ya chapa ya kimataifa, huku akifichua kuwa kampuni yake tayari imetoa asilimia 30 ya fedha za mwaka wa kwanza wa mkataba kama ishara ya kujitoa kikamilifu katika uwekezaji huo.
“Kwa mara ya kwanza Simba Sports Club itakuwa klabu ya kwanza Tanzania kuvaa jezi ya international brand. Tumewekeza fedha nyingi sana kuhakikisha Simba inapata thamani kubwa kulingana na ukubwa wake,” alisema CPA Rwegasira.
Mageuzi hayo pia yamegusa timu za vijana na wanawake za Simba, ambazo kwa sasa zinafanya mazoezi katika viwanja vya kukodi. Ahmed Ally amesema viwanja hivyo vitakuwa historia, kwani klabu hiyo sasa inajenga miundombinu yake ya kudumu itakayohudumia timu zote za Simba kwa kiwango cha kitaalamu.
“Timu ya vijana na timu ya wanawake kwa sasa zinafanya mazoezi kwenye viwanja vya kukodi. Ni senior team pekee ndiyo ipo Mo Simba Arena. Wanaokodisha waanze kutafuta wateja wengine,” alisema kwa msisitizo.
Simba SC, ambayo tayari imeonesha mafanikio makubwa ndani na nje ya uwanja, inatarajiwa kuimarika zaidi kupitia hatua hizi za kimkakati zinazolenga kuimarisha utendaji, kuongeza mapato, na kuinua hadhi ya klabu hiyo hadi viwango vya klabu bora barani Afrika.



