SIMBA imemaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa kileleni mwa msimamo baada ya kuifunga Singida Black Stars kwa bao 1-0 Uwanja wa Liti, Singida jana.
Ushindi huo umeiwezesha Simba kufikisha pointi 40 baada ya kucheza michezo 15, ikishinda michezo 13, sare mmoja na kufungwa mmoja.
Singida Black Stars wanaendelea kushika nafasi ya nne wakiwa na pointi 33 baada ya kucheza michezo 16, wakifungwa michezo miwili, sare mitatu na kushinda michezo 11.
Bao pekee la Wekundu wa Msimbazi lilifungwa na Fabrice Ngoma dakika ya 42 kwa kichwa, akimalizia mpira wa kona uliopigwa na Jean Ahoua na kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, timu zote wakishambuliana huku Singida wakicheza faulo nyingi zilizosababisha mwamuzi, Shomari Lawi kuwaonya kwa mdomo na wakati mwingine kwa kadi ya njano.
Hata hivyo golikipa wa Simba, Moussa Camara aliokoa mpira uliopigwa kwa kichwa na Elvis Rupia akimalizia pasi kutoka kwa Josephat Bada.