TIMU ya soka ya wanawake ya Simba Queens, leo itaivaa AS Kigali katika mechi ya nusu fainali ya kuwania kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).
Mechi hiyo inatarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi Dar es Salaam na kocha wa Simba, Sebastian Nkoma ameiambia Daily News Digital kuwa imani yake leo atafuzu fainali.
Alisema malengo yao ni kufuzu fainali na kukata tiketi ya kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa kwa wanawake ambayo inafanyika kwa mara ya pili.
“Malengo yetu ni kuwa mabingwa hivyo mchezo wa kesho (leo) tumeupa kipaumbele na kwa jinsi ninavyokiona kikosi changu kinanipa matumaini, pia tunataka kulinda rekodi ya kutokufungwa,” alisema.
Simba imefuzu nusu fainali kutoka Kundi B baada ya kuifunga She Corporate ya Uganda kwa mabao 2-0, Garde Republicane ya Djibouti kwa mabao 6-0 na Yei Joints Stars ya Sudan Kusini mabao 4-0 na timu nyingine iliyofuzu kutoka kundi hilo ni She Corporate.
Kutoka Kundi A zilizofuzu ni Commercial Bank FC ya Ethiopia ambao pia watacheza nusu fainali leo dhidi ya She Corporate ya Uganda.
Garde Republicane imeaga mashindano ikiwa imefungwa mabao 20-0 katika michezo mitatu na Yei Joints Stars inaondoka na pointi tatu ilifunga mabao sita na kufungwa mabao 10.
Michezo ya kutafuta mshindi wa tatu na fainali zitachezwa Jumamosi wiki hii.
Michuano hiyo inadhaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan tangu ilipoanza kufanyika mwaka jana.