Simba Queens wapania kumaliza kwa kishindo

DAR ES SALAAM – KOCHA Mkuu wa Simba Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi’ amesema licha ya kuwa tayari wameshatwaa ubingwa hawatapenda kuona wanachafua sherehe zao za ubingwa kwa kufungwa na Geita Queens.

Akizungumza Dar es Salaam jana mshambuliaji huyo wa zamani wa wekundu hao wa Msimbazi, alisema watataka kumaliza ligi kwa ushindi hivyo hawako tayari kuona wanapoteza mchezo wa mwisho dhidi ya Geita Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

“Tungependa kukamilisha msimu wetu kwa ushindi na wala hatutamwonea huruma yeyote, tunataka kumaliza ligi kwa ushindi na kwenda kwenye sherehe za kukabidhiwa kombe tukiwa na furaha ya ushindi,” alisema Mgosi ambaye amewahi kuitumikia Mtibwa Sugar kabla ya kujiunga na Simba.

SOMA: Bajeti 2024/25: Serikali yazibeba VAR

Simba Queens, mabingwa wapya wa ligi hiyo kwa msimu wa 2023/2024 watakabidhiwa kombe baada ya kutamatika kwa ligi hiyo, michezo yote inachezwa saa 10:00 jioni ikiwa ni kuepuka upangaji wa matokeo.

Licha ya kuwepo kwa makabidhiano ya kombe la ubingwa lakini masikio na macho ya wadau wa soka la wanawake yapo kwenye mechi mbili kwa kuwatazama washambuliaji wawili wa timu mbili tofauti, Aisha Mnuka (Simba Queens) akifunga mabao 19 na Stumai Abdallah wa JKT Queens akitikisa nyavu mara 18.

Michezo mingine kwenye ligi hiyo ni JKT Queens dhidi ya Ceassia Queens katika Uwanja wa Samora, Iringa, Fountain Gate Princess dhidi ya Bunda Queens katika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, Amani Queens watawakaribisha Baobab Queens, Uwanja wa Ilulu, Lindi na Yanga Princess watakuwa nyumbani dhidi ya Alliance Girls.

Habari Zifananazo

Back to top button