Simba wanapitia makubwa nyie!

DAR ES SALAAM; SIMBA wanapitia makubwa nyie basi tu! Pengine hivyo ndivyo unavyoweza kuzungumzia hali ya mashabiki wa klabu ya Simba ya Dar es Salaam kwenye mitandao ya kijamii tangu kufunguliwa kwa dirisha la usajili wa wachezaji msimu wa mwaka 2025/26 mapema mwezi huu.
Wanapitia makubwa kutokana na kikosi chao kilichocheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa mwaka 2024/25, ambacho pia kimeshika nafasi ya pili Ligi Kuu Tanzania Bara kuendelea kumeguka kwa kasi, ambapo jana jioni nahodha wa timu hiyo, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ naye alitangaza kumalizana na klabu hiyo baada ya kuitumikia kwa misimu 11.

Wachezaji wengine ambao pia wameachana na Simba ni viungo Fabrice Ngoma, Debora Fernandes, Augustine Okejepha, mabeki Hussein Kazi, Kelvin Kijili na kipa Aisha Manula. Baadhi ya nyota hao mikataba yao imemalizika.
“Msimu uliopita tulisema tunajenga timu, sasa timu tunayoijenga ndo inabomoka, yaani tumemuachia nahodha ameondoka?” Hayo ni baadhi ya maneno ya wanazi wa Simba kwenye makundi mbalimbali ya mitandao ya kijamii, baada ya tamkoa la Tshabalala jana.

Jana katika taarifa yake ya kuaga, Tshabalala alisema uamuzi wake ni kutokana na maslahi yake binafsi, maendeleo yake binafsi na weledi uliotukuka.



