Simba, Yanga zamuunga mkono Karia uchaguzi TFF

KLABU za Simba na Yanga zimepitisha azimio la pamoja la kuunga mkono Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia katika uchaguzi ujao.
Akitoa hoja hiyo Rais wa Simba, Mangungu ambaye alisimama baada ya Mkutano Mkuu wa kawaida kumaliza aliomba wajumbe wenzake kumpitisha Karia kuwa mgombe pekee katika uchaguzi ujao kutokana na maendeleo makubwa aliyofanya kwa soka la Tanzania.
“Wajumbe wenzangu naomba tupitishe azimio la pamoja la kumpitisha Karia kuwa Rais wa TFF sisi kwenye uchaguzi tuje kuchagua wajumbe tu kutokana na kazi kubwa aliyofanya kwa mpira hii ndo zawadi tunaweza kumpatia” alisema Mangungu.
Kauli ya Mangungu iliungwa mkono na Rais wa Yanga, Hersi Saidi na kusema Rais Karia anafaa kupitishwa kugombea urais katika uchaguzi ujao kama alivyo sema Mangungu na yeye hana pingamizi
Baada ya wajumbe hao kutoa hoja wajumbe wenzao walipiga makofi kuonesha wanakubaliana nao lakini Rais Karia akaomba Makamu wa Kwanza wa TFF, Athuman Nyamlani ambaye kitaaluma ni mwanasheria kutoa ufafanuzi kuhusu hoja hiyo.
Nyamlani alisema kwa sasa kusema kumpitisha Karia kuwa mgombea pekee watakuwa wanakwenda kinyume na Katiba ya TFF inayozungumzia utawala bora badala yake kipindi cha uchaguzi kikifika wanachama wa TFF ndo wampitishe.
“Kwa sasa tutakuwa tunapingana na dhana ya utawala bora ila kipindi cha uchaguzi kikifika wanachama mnaweza kufanya hivyo, na si dhambi maana duniani kote inafanyika” alisema Nyamlani.
Alitolea mfano Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) Patrice Motsepe na Rais wa Fifa, Inflantino walishawahi kupitishwa na wanachama wao.



