Simulizi ya maisha ya Cleopa Msuya nyumbani

JUNI 2023 Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya (amefariki juzi) alifanya mahojiano na timu ya waandishi wa habari wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) waliofi ka nyumbani kwake na kuzungumzia mambo kadhaa.
Fuatilia mfululizo wa makala kuhusu mambo mbalimbali binafsi na ya kitaifa aliyozungumza. Juni 6, 2023 timu ya waandishi wa habari wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) ilifika katika Kijiji cha Chomvu, Kata ya Usangi wilayani Mwanga, Kilimanjaro kwa mahojiano maalumu na Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya.
Katika mahojiano hayo, Msuya anaweka bayana maisha yake ya nyumbani, elimu,ajira na nyadhifa mbalimbali alizoshika nchini. Mwenyewe anasema alishika wadhifa wa waziri mkuu mara mbili chini ya marais wawili tofauti.
Kwamba, mara ya kwanza ilikuwa kuanzia Novemba 7, 1980 hadi Februari 24, 1983 chini ya Urais wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Anasema mara ya pili ilikuwa Desemba 5, 1994 hadi Novemba 28, 1995 huku akishika pia wadhifa wa Makamu wa Kwanza wa Rais chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi.
Mstaafu huyu ambaye pia aliongoza wizara mbalimbali ama akiwa katibu mkuu au waziri, miongoni mwa  alizoongoza kwa ufanisi ni pamoja na Wizara ya Viwanda aliyoiachia alama ya viwanda mbalimbali.
Maisha nyumbani, elimu na ajira.
Akielezea maisha ya nyumbani, elimu na ajira katika mazungumzo hayo, Msuya anasema baba yake, David Kilenga na mama yake, Maria Mgido walimzaa akiwa mtoto wa tano kati ya watoto 10. Kwamba, waliishi maisha ya kawaida katika mazingira ambayo wazazi wanajitegemea.
“Sisi tulikuwa watoto 10 kwa mzee wetu na mama… Nimebaki mimi tu. Lakini tulivyolelewa ni kwamba, usiku mkishafanya shughuli zile za kutwa, mnakula chakula na mnaomba (mnasali) kabla ya kwenda kulala maana wazee wangu walikuwa Wakristo.”
“Lakini na kazi zinapangwa, kwamba sasa kesho watoto mtafanya nini. Wale wakubwa wanapangiwa kazi zao, sisi wadogo tunapangiwa kazi zetu.” “Tunaokwenda shule tunapangiwa kazi ambazo zinakidhi mahitaji ya shule na kuhudumia mifugo au kitu namna hii,” anasimulia.
Anaendelea na simulizi: “Tumeishi maisha hayo mpaka nikamaliza shule ya msingi, darasa la nne mwaka 1943 hapa Usangi. Nimesoma Kimedu mwaka 1942 nikarudia pale NA (Native Authority) mwaka 1943. Zamani shule za Native Authority zilikuwa chache, moja ilikuwa hapa Usangi na nyingine Msangeni, Ugweno.”
Baada ya hapo, anasema alifanya mtihani akabahatika kwenda Old Moshi mwaka 1944 kuanza Darasa la Tano hadi Darasa la 10 alipofanya mtihani.
“Wakati ule Old Moshi ilikuwa inachukua watoto wengi kutoka sehemu hii ya North Pare, South Pare na Wachanga na vijana wengine kutoka Arusha, tukafanya mtihani. Bahati nikachaguliwa, nikafaulu nikaenda Tabora mwaka 1950/1951 tukasoma miaka miwili pale Tabora High School. Tukafanya mtihani wa Cambridge, bahati nikafaulu. Nikachaguliwa kwenda Makerere,” anaeleza.
Anaendelea kusimulia, “Kwa hiyo ikabidi kwenda Makerere… Sijui kama mnafahamu kilikuwa ni chuo kinapokea watoto kutoka Afrika Mashariki yote na tulikuta watoto wengine kutoka Zambia wengine kutoka Malawi, Ethiopia, Sudan lakini sana sana ilikuwa ni Kenya, Uganda na Tanzania.”
Katika mazungumzo hayo Juni 6, 2023, Msuya anasema alisoma Masomo ya Sanaa katika chuo hicho kilichokuwa kikilelewa na Chuo Kikuu cha London cha Uingereza. Anafahamisha kuwa, shahada zilizokuwa zinatolewa ni za London hazikuwa za Makerere.
Alipata Shahada ya Kwanza ya Sanaa katika Sayansi ya Siasa, Jiografia na Historia 1955. ‘Kandanda’ za ajira “Sasa ikaja kandanda ya kuajiriwa. Baadhi yetu tulitaka tuingie kwenye ‘administrative system’ (mfumo wa utawala). Unajua baadhi yetu wakati wa ukoloni, watu wanaoshika madaraka makubwa ni ‘administrative officers’ (maofisa utawala) ambao ni ma-DC (wakuu wa wilaya) na chini yao ni ma- district officers (maofisa wa wilaya).”
Anasema alitaka kuingia katika mfumo huo lakini Serikali ya Tanganyika haikuwa inapendelea kuwapokea. Waliwashinikiza wachukue ualimu.
“Tukawaambia sisi wengine hatuna ‘interest’ (hatupendi) ya ualimu.” Nakumbuka tulikwenda kusailiwa na Serikali ya Uganda; wao wakasema kama Serikali ya Tanganyika haipo tayari kukupeni, sisi serikali ya Uganda tupo tayari kuwaajiri huku,” anasema.
Anasema walisailiwa na gavana na sekretarieti yake nchini Uganda. Hata hivyo anasema baadaye kulikuwa makubaliano kwa kile anachosema, wakuu wa Dar es Salaam (Tanganyika), walipeleka habari kwamba wawaambie waende nyumbani.
Kwa mujibu wa Msuya, walikuwa watatu; wengine wakiwa rafiki zake, Dickson Mkembwa aliyekuwa mwenyeji wa Mbeya (sasa ni marehemu) ambaye baadaye alipewa wadhifa wa mkuu wa utumishi na mwingine alikuwa Jeremiah Byarugaba kutoka mkoani Kagera ambao wote hawakutaka kuingia kwenye ualimu.
Akizidi kusimulia anasema waliambiwa warudi nyumbani watajulishwa mahali pa kwenda. “Kwa hiyo tukafunga safari tukarudi nyumbani. Mwaka 1956 mwanzoni nikaletewa barua kwamba nikaripoti Moshi, nimepangiwa kuwa Bwana Maendeleo pale Moshi,” anasimulia.
Anasema alipangwa zaidi kwenye masuala ya vijana kwani wakati ule pia kulikuwa na tatizo la watoto kusoma na kumaliza shule ya msingi kisha elimu inakoma hapo. Kwa hiyo ilibuniwa programu ya vijana ambayo ilibidi kushughulika nayo.
Anasema alikaa ndani ya mwaka na 1957 alipelekwa Tabora na kazi yao kuwa ilikuwa ya kimaendeleo ikiwamo kushawishi wakulima wazalishe mazao. Akataliwa na DC Mzungu Baada ya muda, anasema alihamishwa akaambiwa aende Same; Wilaya ya Pare iliyokuwa inaunganisha Mwanga na Same.
“Pakatokea kasheshe nyingine, inaelekea DC Mzungu mmoja alikuwa hapo Same anaitwa Chant (John), akawa na wasiwasi kwamba mimi nikienda pale ni Mpare (kabila), aliyekuwa ameshika polisi alikuwa Shaidi Elangwa, alikuwa OCD; halafu Izunde alikuwa ‘administrative officer’ (ofisa utawala).
“Sasa nafikiri DC akawa na wasiwasi kwamba tukiingia pale, itatengeneza shinikizo la kisiasa kutoka kwa watu wetu na sisi tunaweza kuwa ni sababu,” anasema. Katika kuzima hilo, badala ya kwenda Wilaya ya Pare, anasema aliambiwa aende Tengeru ambako kulikuwa na chuo chao.
“Pale nikaenda, wakati ugomvi huo ulitokana na DC na makao makuu yetu kule Dar es Salaam wanabishana kwamba kwa nini, ni ofisa wetu, tunamwamini, atafanya kazi vizuri, wewe una wasiwasi!” anasimulia.
Anasema wakati wa mvutano huo, vitu vyake vilikuwa vimeshakwenda Same huku akisubiri matokeo ya mvutano huo. Baadaye alirudi na mwaka 1959 akaoa. Akiwa wilayani humo, badala ya kupangiwa Same mjini, walimuacha afanyie eneo la Mamba.
Kazi kubwa waliyokuwa nayo ilikuwa ni kuongeza uzalishaji wa kahawa huku akishirikiana na Bwana Kilimo kupanua barabara ziwafikie wakulima sehemu za mbalimbali kwa ushawishi wa msaragambo; kabla ya kurudi Same.Mwaka 1960, ambao vuguvugu la kupata uhuru lilipamba moto, aliambiwa aendeDar es Salaam baada ya wakoloni kuamua kuwachukua Watanganyika wenye elimuwajifunze jinsi ya kuendesha wizara.
Hiyo ilikuwa tiketi yake ya kuchomoza na hatimaye kuingia kwenye wizara tofauti; Wizara ya Ardhi, Maji na Makazi, Wizara ya Uchumi na Mipango, Wizara ya Viwanda, Wizara ya Fedha na Wizara ya Viwanda ambayo ameacha alama kubwa.
Alipata uteuzi wa kwanza wa ubunge kisha kupewa uwaziri wa fedha mwaka 1972. Kabla ya hapo, alikuwa Katibu Mkuu katika Wizara ya Fedha. Mwaka 1975, Nyerere alimteua tena kuwa mbunge na kumpa uwaziri wa viwanda wadhifa aliotumikia hadi 1980.
“Mwaka 1980 nikasimama nikachaguliwa kama Mbunge wa Mwanga na bahati Rais (Nyerere) akanichagua kuwa Waziri Mkuu,” anasema. Baada ya kutumikia taifa katika nyadhifa hizo tofauti, Msuya alistaafu ubunge mwaka 2000.
“Niliacha na niliaga pale bungeni. Niliporudi wilayani wakaniomba niwasaidie nikawa katibu wa chama (CCM), Uchumi na Fedha. Nikaendelea lakini kule kwingine nikaacha.”
Anasema nafasi hiyo katika chama aliiacha mwaka 2010 na kubaki kuwa mwanachama wa kawaida. Shughuli alizoendelea nazo ilikuwa ni kuwa Mwenyekiti wa Kampuni ya Bia (TBL) kwa miaka 15 hadi 2021. Aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete (wa awamu ya nne) kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ardhi kwa miongo miwili hadi mwaka 2021.
Alikuwa miongoni mwa viongozi wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Kilimanjaro Development Forum. Cleopa Msuya alikuwa baba wa watoto sita (akiwamo aliyefariki mwaka 2005).
Fuatilia makala ijayo akisimulia alivyochomoza na kushika madaraka kitaifa.

Habari Zifananazo

One Comment

  1. I was BROKE and desperate… now I make $3,000+ weekly from my couch! Just 30 days ago, I was stuck in a dead-end job, living paycheck to paycheck. Then I found this secret method—and everything changed Anyone can do this in their free time. Spots are LIMITED! Don’t miss out!

    Join now➤➤ 𝐖­𝐰­𝐰­.­𝐄­𝐚­𝐫­𝐧­𝐀­𝐩­𝐩­𝟏­.𝐜­𝐨­𝐦

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button