Singida, Mlandege kitaeleweka

FAINALI ya michuano ya Kombe la Mapinduzi inatarajiwa kuchezwa leo kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar kati ya Singida Big Stars na Mlandege FC.
Mechi hiyo inatarajiwa kushuhudiwa na Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.
Ni mchezo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini baada ya kila timu kuonesha kiwango bora katika michezo ya hatua ya makundi.
Singida ilimchapa Azam FC katika mchezo wa nusu fainali kwa mabao 4-1 na kutinga hatua hiyo, huku Mlandege ikimtoa Namungo kwa mikwaju ya penalti 5-4 baada ya dakika 90 za kutoka sare ya bao 1-1.
Safari za hatua ya makundi zilionesha mapema kwamba ni timu bora, Singida iliyokuwa Kundi B, awali ilimchapa KMKM mabao 2-0 kisha ikatoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Yanga ikiwa imelingana pointi nne ikasonga mbele kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Mlandege iliyokuwa Kundi C iliibuka kinara baada ya kuwafunga Simba bao 1-0, kisha ikapata sare dhidi ya KVZ ya bao 1-1.
Timu zote zinafanya vizuri kwenye ligi zao, Singida ikiongozwa na mchezaji mpya, Francy Kazadi, inashika nafasi ya nne Ligi Kuu Tanzania Bara hivyo haipaswi kubezwa huenda ikaendeleza ushindi kama itaendelea kucheza kwa kiwango ilichoonesha kwenye mechi zake zilizopita.
Kazadi amekuwa na kiwango bora na ni mchezaji hatari baada ya kufunga mabao manne katika mchezo uliopita.
Pia, Mlandege inafanya vizuri ligi ya Zanzibar ikishika nafasi ya tano inaweza kufanya lolote ili kulibakiza kombe hilo na kuwabeba Wazanzibari baada ya timu nyingi za huko kushindwa kulichukua kwa miaka mingi.
Kocha Mkuu wa Mlendege, Abdallah Mohamed, aliwaahidi mashabiki wa soka wajitokeze kwa wingi kuisapoti timu hiyo.
Alisema wamejipanga vizuri na anatamani kuona wanapata ushindi ili kombe libakie Zanzibar.
Kocha Msaidizi wa Singida Big Stars, Mathias Lule alisema kikosi chake kiko tayari na watapambana kufikisha malengo yao.
“Tumejiandaa kuona namna tunaweza kupata matokeo mazuri, kila mchezo una matokeo yake, tunaingia tukijua ni mchezo utakaokuwa mgumu, tutapambana kupata ushindi,” alisema.
Kombe hilo msimu uliopita lilichukuliwa na Simba, pia liliwahi kuchukuliwa na Yanga, Azam FC, Mtibwa na Miembeni.