SMZ yajipanga kuzuia usafirishaji wa binadamu

TAASISI zinazohusika na kuzuia na kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu zimetakiwa kuongeza ubunifu na kutumia mbinu za kisasa kubaini vyanzo vyote vya uhalifu huo, ambao umeendelea kuwaathiri kwa kiwango kikubwa wanawake na watoto nchini.

Wito huo umetolewa leo, Novemba 26, 2025, na Mkurugenzi wa Uratibu wa Shughuli za Serikali, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Siajabu Suleiman Pandu, wakati akifungua Kikao cha Wadau wa Serikali cha kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano katika mapambano dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu, kilichofanyika Mwembe Madema, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Akizungumza katika kikao hicho, Pandu amesema jamii inapaswa kutoa taarifa za matukio yanayohusiana na usafirishaji haramu wa binadamu kwa vyombo vya dola ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa. “Vita dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu haiwezi kufanikiwa bila ushiriki wa wananchi. Taarifa sahihi kutoka kwa jamii ni msingi wa kuchukua hatua za haraka na madhubuti,” alisema.

Kwa upande wake, Afisa Mwandamizi wa Sekretarieti ya Kuzuia na Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu, Rafii Said Mnete, amesema Serikali kupitia Sekretarieti hiyo imejipanga kuboresha mikakati na kuchukua hatua thabiti za kukabiliana na vitendo hivyo, ikiwemo kuimarisha ufuatiliaji, elimu kwa umma na ushirikiano wa taasisi. “Tunazidi kuongeza nguvu katika maeneo yote muhimu kuzuia, kutambua na kuchukua hatua. Huu ni uhalifu mtandao unaohitaji ushirikiano mpana,” alieleza.

Naye Naibu Katibu wa Sekretarieti hiyo, Kanda ya Zanzibar, Huzaimat Bakar Kheir, amesema lengo la kuzikutanisha taasisi hizo ni kuimarisha uratibu na kubadilishana taarifa ili kuongeza ufanisi katika kupambana na uhalifu wa usafirishaji haramu wa binadamu. “Ushirikiano wa taasisi ni silaha muhimu. Kupitia majadiliano haya tunaweka msingi wa hatua za pamoja zenye matokeo ya haraka,” alisema.

Kikao hicho kimehusisha taasisi mbalimbali za Serikali kutoka Zanzibar na Tanzania Bara, zikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama, mamlaka za udhibiti, na idara za ustawi wa jamii. SOMA: Uhamiaji wakabidhiwa gari kudhibiti wahamiaji haramu

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button