Spika atoa maekezo waathirika matrekta ya Ursus
DODOMA; SPIKA wa Bunge, Dk Tulia Ackson ametoa maelekezo kwa serikali kuchambua na kubainisha makundi mbalimbali ya wakulima walioathirika kutokana na mradi wa kuwakopesha matrekta na kuonesha namna ya kuwapatia nafuu waathirika hao.
Ametoa kauli hiyo leo bungeni, alipokuwa akitoa uamuzi kuhusu taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo kuhusu Changamoto na Malalamiko yaliyojitokeza katika kutekeleza mkataba wa mauziano ya matrekta ya Kampuni ya Ursus kati ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na wakulima kwa utaratibu wa mikopo.
Dk Tulia amesema ataikabidhi taarifa yote ya kamati hiyo kwa serikali ili ifanyiwe kazi mapendekezo yote ya kamati na maagizo mahususi, kisha ripoti ikikamilika itapelekwa kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ili ifuatilie kwa karibu utekelezaji wa changamoto hizo.
Akizungumzia taarifa ya kamati, Dk Tulia amesema imeeleza kuwa yapo makundi mbalimbali katika mkataba huo, ambapo lipo kundi ambalo lilishamaliza kulipa madeni, lakini lipo ambalo limelipa sehemu ya deni na lipo ambalo halijalipa kabisa.
Amesema hata mikataba waliyoingia haifanani baina ya kundi moja na lingine, hivyo hata mfumo wa marejesho unatofautiana.
Dk Tulia ameitaka tume iliyoundwa na serikali kuhusu suala hilo mwaka 2019, kukamilisha kazi yake na kutoa mrejesho inavyotakiwa, ili taarifa ifikie hatua nyingine ya kuwakwamua wakulima walioathirika.
Pia ameagiza taarifa zote zinazotakiwa na kamati ziwasilishwe kwa Katibu wa Bunge na hilo lifanyike kabla ya vikao vya kamati za bunge mwezi Oktoba ili izifanyie kazi.
Baadhi ya ripoti hizo ni ripoti ya ukaguzi uliofanywa na kituo cha Kamatek kuhusu dosari kwenye matrekta ya Ursus, ripoti ya makabidhiano ya mradi kutoka SumaJKT kwenda NDC, ripoti ya kikao cha timu ya serikali ya majadiliano na ripoti ya Wizara ya Fedha kuhusu malipo ambayo yameshafanyika.