Soko Kuu Mwanza katika hatua za mwisho kufunguliwa

UJENZI wa Soko Kuu katikati ya Jiji la Mwanza umefikia asilimia 80 huku kazi ikiendelea kwa kasi kuhakikisha kwamba linaanza kutumika mwezi ujao kama mkataba ulivyoainisha.

Hayo yamebainishwa na Mhandisi wa Kampuni ya Mohammed Builders, John Peter wakati akizungumza na HabariLEO.

“Kwa sasa kazi kubwa iliyobakia ni kuweka paa, hivyo tuna uhakika wa kukamilisha ujenzi wa soko hapo mwezi ujao,” alisema Mhandisi Peter.

Alisema wameshaandaa mazingira hitajika kwa ajili ya kuwezesha uwekaji wa paa kwenye jengo hilo kubwa hapa nchini.

Soko hilo ambalo ni ghorofa moja lina ukubwa wa square meta 28,000 na litakuwa na maduka 398 kwa upande wa juu na chini 72, vizimba 332 vya matunda, vizimba 372 vya nafaka.

Mhandisi Peter aliongeza kusema kuwa kutakuwa na eneo la magari 392 ya wateja wanaofika kununua bidhaa katika eneo hilo kwa wakati mmoja na eneo la kuuzia bidhaa wafanyabiashara wadogowadogo 217.

Aliongeza kusema kuwa soko hilo litakuwa na eneo kubwa la mkahawa, vyumba 15 vya stoo kubwa kwa ajili ya kutunzia bidhaa mbalimbali.

Baadhi ya wananchi wakizungumzia ujenzi huo kwa kusema kuwa utafanya Jiji la Mwanza kuwa na mwonekano mzuri unaoendana na hadhi ya jiji na wakati huo huo kuwezesha Watanzania kuuzia bidhaa zao katika eneo hilo ambalo ujenzi wake umeanza Oktoba, 2020.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button