WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesema iko katika hatua za ukamilishaji wa mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 na Mitaala katika ngazi ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Mafunzo ya Ualimu.
Kauli hiyo imetolewa bungeni leo na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omari Juma Kipanga, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Zainabu Katimba aliyetaka kujua lini serikali itaboresha mitaala ya elimu ili mafunzo ya biashara yatolewe kuanzia shule za msingi.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Kipanga amesema wizara imevielekeza vyuo vikuu kuhuisha na kufanya maboresho ya mitaala yote, ili iendane na Dira na Mipango ya Maendeleo ya Taifa katika kutoa elimu itakayompa kijana wa Kitanzania ujuzi.
“Wizara inatambua umuhimu wa somo la biashara na hivyo somo hili limepangwa kuwa ni somo la lazima kwa wanafunzi wote kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne kwa mikondo yote miwili ya Elimu ya Jumla na Elimu ya Amali.
“Kwa Ngazi ya Elimu ya Msingi Darasa la I-VI mitaala imetilia mkazo elimu ya fedha pamoja na elimu ya ujasiriamali, ambapo elimu ya fedha imechopekwa kwenye somo la Hisabati na Elimu ya Ujasiriamali imechopekwa kwenye somo la Sanaa na Michezo, lugha, Jiografia na Mazingira.
“Mheshimiwa Spika, vyuo vikuu vya serikali na binafsi kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa mageuzi ya kiuchumi (HEET) vimepata mafunzo mbalimbali ya kuandaa programu zinazoendana na vipaumbele vya nchi na mahitaji ya soko la ajira.
“Kupitia utaratibu huu, zaidi ya programu 300 zitaanzishwa au kuhuishwa ikiwemo somo la biashara ili kuendana na mahitaji ya sasa ya kijamii, kiuchumi na soko la ajira,” amesema Naibu Waziri.