Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Dk Fredrick Sagamiko amesema matumizi ya Chombo Maalum cha Madhumuni (Special Purpose Vehicle- SPV) ni njia bora ya usimamizi na uendeshaji wa miradi ya vitega uchumi vya Halmashauri ili kufikia lengo maalumu lililokusudiwa kwa kuanziashwa kwa vitega uchumi hivyo ikiwemo kutoa huduma kwa wananchi na kukusanya mapato kwa Halmashauri.

Dk Sagamigo amesema hayo katika kikao kazi cha maandalizi ya mpango na bajeti kwa mwaka 2025/26 kwa wataalamu wa mipango kutoka ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kinachoendelea jijini Dodoma.

Amesema SPV ni chombo cha kisheria (kampuni) inayoanzishwa kwa ajili ya kusimamia shughuli mbalimbali zikiwemo za kibiashara na uzalishaji katika taasisi husika ikiwemo Mamlaka ya Serikali za Mitaa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sera na Mipango Ofisi ya Rais TAMISEMI, John Mihayo Cheyo amesema Serikali imekwisha kuandaa miongozo maalumu kwaajili ya usimamizi na uendesheja wa vituo vyote SPV katika Halmashauri zote nchini.