Stanchart yakamilisha uhamishaji wa biashara za kibenki kwa Access

DAR ES SALAAM: BENKI ya Standard Chartered Tanzania imekamilisha uhamishaji wa biashara zake za huduma za kibenki kwa wateja wa hali ya juu na wa kawaida (rejareja) kwenda kwa Access Bank PLC.

Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kimataifa wa benki hiyo wa kuongeza ufanisi, kupunguza ugumu wa uendeshaji, na kuongeza uwezo wa utoaji huduma kwa wateja wengi zaidi.

Hayo yamesemwa Dar es Salaam ambapo imeelezwa uhamishaji huo unaashiria kufungwa kwa sura ya huduma za benki ya rejareja ya Standard Chartered nchini Tanzania, kufuatia uamuzi wake wa kimkakati uliotolewa Aprili 2022 wa kujiondoa katika baadhi ya masoko barani Afrika, likiwemo soko la huduma za kifedha kwa watu binafsi na wenye utajiri.

Akizungumza katika hafla ya kutangaza kukamilika kwa uhamishaji huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Standard Chartered Tanzania, Herman Kasekende, alisema hatua hiyo ni sehemu ya mabadiliko ya kimkakati ya benki hiyo duniani kote.

“Mabadiliko haya ni hatua muhimu tunapojielekeza upya katika maeneo yetu ya msingi ya kiutendaji. Kipaumbele chetu kimekuwa kuhakikisha mabadiliko haya yanafanyika kwa ustawi wa wafanyakazi na wateja wetu, ambao ndio msingi wa kila tunachofanya. Tuna imani kuwa chini ya Access Bank PLC, wateja wetu wa rejareja pamoja na wafanyakazi wataendelea kupata huduma bora kama walivyozoea,” alisema Kasekende.

Licha ya kujiondoa katika sekta ya huduma za wateja binafsi na rejareja, Standard Chartered imesisitiza kuwa itaendelea kuwepo nchini Tanzania, kwa kuwekeza zaidi katika huduma za benki kwa makampuni na uwekezaji (Corporate and Investment Banking), ambazo zinaendelea kuwa sehemu ya mkakati wake wa muda mrefu barani Afrika.

Benki hiyo, ambayo imekuwa ikihudumu nchini tangu mwaka 1917, imeeleza kuwa itaendelea kuwa mshirika wa karibu wa makampuni, taasisi na serikali katika kukuza uchumi wa taifa.

Uhamishaji huo umefungua ukurasa mpya kwa Access Bank PLC, ambayo sasa inapanua wigo wake wa huduma kwa kuwakaribisha rasmi wateja wa zamani wa Standard Chartered pamoja na wafanyakazi waliokuwa sehemu ya idara ya rejareja na huduma kwa watu binafsi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button