SUA kuakisi maendeleo

MOROGORO: CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kimetajwa kuchangia maendeleo nchini kwenye nyanja mbalimbali kutokana na wataalamu wanaofundishwa wa kizazi cha sasa na kijacho.
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Raphael Chibunda amesema hayo kwenye ufunguzi wa mafunzo ya uongozi kwa viongozi na watumishi yaliyoandaliwa na chuo hicho.
Profesa Chibunda amesema,wote ambao wameaminiwa kuwa watumishi wa chuo hicho na waliopata nafasi za uongozi wanapaswa kuwa na nia dhabiti ya kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na weledi mkubwa.
“Waliopata nafasi ya uongozi wasilichukulie kuwa ni suala rahisi bali mnapaswa muwe na nia dhabiti na kutekeleza majukumu ambayo mmekabidhiwa kwa uwezo wenu wote “ amesema Profesa Chibunda.
Profesa Chibunda amesema hayo yote ni katika kuwezesha jukumu ambalo taifa limekikabidhi chuo hicho kufundisha wataalamu wa waleo na wajao.
Ameongeza kuwa jambo hilo linapaswa lifanyike kwa ufanisi mkubwa kama ambavyo serikali inavyotegemea.
Naye Katibu Msaidizi Maasili ya Viongozi, Fabian Pokela akiwasilisha mada Kanuni za Maadili ya Utumishi wa Umma amesema uadilifu kwa viongozi na watumishi wa umma yanachangia kuleta utendaji wenye ufanisi kwenye Taasisi za umma nchini.
Kwa upande mnufaika wa mafunzo hayo ,Rasi wa Ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii wa Chuo Kikuu hicho , Profesa Agnes Sirima amesema mafunzo hayo ni muhimu kwake akiwa kiongozi kuyapata kwa sababu yatamsaidia kutekeleza vyema majukumu yake ya kila siku ili yaweza kuleta tija.