SUA wasaini mikataba ujenzi wa majengo mapya mradi wa HEET

CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeanza ujenzi wa majengo mapya na kufanya ukarabati katika maeneo mbalimbali baada ya kupokea Sh bilioni 41 .1 zilizotolewa na Serikali kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).

Mradi wa HEET kwa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi ni utekelezaji wa azma ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia.

Makamu mkuu wa Chuo Kikuu hicho, Profesa Raphael Chibunda amesema hayo wakati wa kusaini mikataba na wakandarasi wakiwemo wazawa na wakichina kuhusu ujenzi wa majengo saba mapya yenye madarasa. Maabara ,kumbi za mikutano na kufanya ukarabati wa majengo mbalimbali na miundombinu mingine.

Advertisement

Profesa Chibunda alisema mradi unatarajia kukamilika ndani ya miezi 18 kuanzia sasa na umelenga kuboresha mazingira ya kujifunzia ,kuboresha mitaala kwa kuzingatia soko la ajira na kuongeza ubora wa usimamizi wa elimu ya juu.

Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu hicho amesema mradi utaimarisha Kampasi ya Edward Moringe ambayo ni kampasi kuu pamoja na kampasi ya Solomon Mahlangu iliyopo Mazimbu kwa kuboresha mazingira ya kujifunzia .

Pia amesema mradi huo utahusika na ujenzi wa kumbi za mihadhara ,hostel za wanafunzi, maabara, karakana za uhandisi, ofisi za watumishi na maeneo mengine muhimu ya kujifunzia na kujifundishia.

Profesa Chibunda amesema kuwa miradi hiyo imegawanyika katika sehemu kuu tatu na itagharimu jumla ya Sh bilioni 41.1 na kati ya fedha hizo Sh bilioni 39.5 ni gharama za wakandarasi na Sh bilioni 1.4 ni gharama za washauri waelekezi .

Amesema kwa Kampasi ya Edward Moringe ,Chuo kitajenga majengo matano ambayo yatagharimu Sh bilioni 19.2 likiwemo na jengo la taaluma litakaokuwa na uwezo wakuchukua wanafunzi 3,500 kwa wakati mmoja.

Naye Kiongozi wa ujenzi wa mradi HEET kitaifa kutoka Wizara ya Elimu ,Sayansi na Teknolojia , Mhandisi, Hanington Kagiraki amesema kuwa wanatarajia mradi ukamilike kwa wakati kwa kuzingatia ubora na uwepo wa vifaa husika.

“Kama jengo la maabara linapokamilika tunatarajia kuona jengo na vifaa vyake vikiwemo ,ikiwa ni darasa au hosteli pia vifaa vyake viwemo amesema Mhandisi Kagiraki.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Morogoro Adam Malima ambaye alikuwa ni miongoni mwa walioshuhudia utiaji wa saini wa mikataba hiyo amesema Serikali ya mkoa itahakikisha inashirikiana na SUA kuhakikisha kuona miradi hiyo inakamilikwa kwa wakati .