Sudan Kusini yasitisha mitandao ya kijamii

SUDAN KUSINI : SERIKALI ya Sudan Kusini imeamua kusitisha huduma za mitandao ya kijamii kwa mwezi mmoja, ikiwa ni hatua ya kukabiliana na machafuko yaliyosambaa nchini humo.

Uamuzi huu ulifanywa baada ya kusambaa kwa video zinazoonyesha kile kinachosemekana kuwa mauaji ya raia wa Sudan Kusini katika jimbo la El Gezira.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini humo, Napolepon Adok, alitangaza kuwa hatua hii imeanza rasmi Jumatano, tarehe 22 Januari 2025.

Katika taarifa yake, Adok alisema kuwa uamuzi wa kufunga mitandao ya kijamii umetokana na machafuko ya hivi karibuni nchini humo ambayo yamechochea ukatili mkubwa, huku mitandao ya kijamii ikiwa ni sehemu muhimu ya kusambaza taarifa na picha za vurugu hizo.

Watumiaji wa huduma za simu kupitia kampuni za MTN na Zain nchini humo hawataweza kupata huduma za Facebook, TikTok, na mitandao mingine kwa kipindi cha hadi siku 90.

Hatua hii inajiri baada ya ghasia kuibuka katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, na maeneo mengine nchini humo, ambapo karibu raia 16 waliuawa wiki iliyopita.

Uamuzi huu unalenga kudhibiti usambazaji wa taarifa na picha zinazoweza kuchochea ghasia zaidi, huku pia ukilenga kupunguza athari za machafuko yanayoendelea nchini humo.

SOMA: Sudan Kusini waahirisha uchaguzi Desemba 2026

Habari Zifananazo

Back to top button