SUDAN: Tom Fletcher ataka hatua za haraka kukabiliana na mzozo

SUDAN : MKUU wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya kibinadamu Tom Fletcher ametoa wito kwa mashirika ya kimataifa kuchukua hatua za haraka ili kudhibiti mzozo unaozidi kuongezeka nchini Sudan.

Fletcher amesema mzozo huo umechangia  kuongezeka kwa mateso ya mamilioni ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na mgogoro huo wa kivita nchini humo.

Tom Fletcher amezungumza na wakimbizi wakati wa ziara yake ya siku tisa katika nchi za Sudan na Chad, na kuapa kuweka wazi madhila yao na kuzitaka nchi zote duniani kutoa msaada zaidi.

Fletcher amesisitiza kuwa takriban watu milioni 26 ikiwa ni karibu nusu ya wakazi wa Sudan, wanakabiliwa na tatizo la njaa huku pande zote mbili zinazopigana zikitumia tatizo la njaa kama silaha ya vita.

Sudan imekumbwa na vita tangu Aprili mwaka 2023, kati ya jeshi la taifa linaloongozwa na Abdel-Fattah al-Burhan na vikosi vya RSF, vinavyoongozwa na Mohamed Hamdan Daglo.

Vurugu hizo zimesababisha vifo vya maelfu watu na kuwafanya zaidi ya wengine milioni 11 kuwa wakimbizi ndani ya nchi yao. SOMA: Urusi yazuia azimio la kusitisha vita Sudan

Umoja wa Mataifa unauelezea mzozo huo kuwa janga baya zaidi la kibinadamu katika historia ya hivi karibuni.

 

Habari Zifananazo

Back to top button