Sukari ya nje kuingia mwezi huu kuziba upungufu

SERIKALI imetoa vibali vya kuagiza nje ya nchi sukari tani 50,000 ili kukabiliana na uhaba wa bidhaa hiyo na zitaanza kuwasili mwezi huu.

Sukari imekuwa adimu nchini kiasi kwamba bei imepanda kufikia kati ya Sh 3,200 mpaka Sh 4,000 kutoka Sh 2,500 hadi 3,200.

Mkurugenzi wa Bodi ya Sukari nchini, Profesa Kenneth Bengesi alisema jana kuwa sukari hiyo inaagizwa kama dharura na inatarajiwa kuingia wakati wowote kuanzia katikati ya mwezi huu.

Advertisement

“Hatutarajii tatizo hili la sukari likachukua zaidi ya wiki mbili kutoka sasa kwa sababu tayari viwanda vimeshaanza uzalishaji,” alisema Bengesi.

Alisema kwa sasa hawezi kusema kiasi gani cha sukari kinahitajika nchini kwa sababu hawajafanya tathmini.

“Mara nyingi huwa tunafanya tathmini Machi viwanda vinapofungwa kupisha hali ya hewa, lakini kwa hili lililotokea hatuwezi kujua kwa sasa…na unajua hizi mvua za Novemba na Desemba ndio zimesababisha hili na hatukujiandaa kwa sababu zilitushtukiza,” alifafanua mtendaji Bodi ya Sukari.

Juzi bodi iliviagiza viwanda vya sukari vya Kagera, Mtibwa, Bagamoyo, Kilombero, TPC na Mkulazi kuanza uzalishaji kwa vile hali ya hewa imetengamaa.

“Kwa hiyo uzalishaji utakapoanza na sukari itakayoagizwa nje ikifika itaunganishwa kwenye soko, hali itakuwa shwari huku uzalishaji ukiendelea,” aliongeza.

Upungufu wa sukari umetokana na upungufu wa bidhaa hiyo kwenye maghala kulikosababishwa na viwanda kusimamisha uzalishaji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Bengesi alisema baada ya viwanda kusimama uzalishaji, sukari iliyokuwa inatumika ni iliyozalishwa Mei na hivyo kusimama kwa uzalishaji kulimaanisha sukari iliyokuwepo kwenye maghala imepungua kwa kiasi kikubwa hali iliyofanya wafanyabiashara wasio waaminifu kutumia mwanya huo kupandisha bei.