SUMA JKT, Comoro kuendeleza biashara

SHIRIKA la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA-JKT) limeingia makubaliano ya kibiashara na Kisiwa cha Ngazidja nchini Comoro ili kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara uliopo baina ya nchi hizo mbili.
Makubaliano hayo yamesainiwa leo Oktoba 12,2024 na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Suma-JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele na Gavana wa Kisiwacha Ngazidja Nchini Comoro, Mze Mohamed Ibrahim katika makao makuu ya Suma JKT Dar es salaam.
Mabele amesema ushirikiano baina ya nchi hizo mbili ni ya kihistoria kabla hata ya uhuru pia kutokana na jamii hizo kushabihiana kwa mambo mengi kama mila, asili vyakula na mengineyo.
“Kama sehemu ya kutafuta fursa kwenye biashara tulienda katika visiwa vya Comoro na wenzetu wametukaribisha kwenda kufanya nao biashara kwahiyo wametukaribisha kufanya kazi katika biashara mfano ya ujenzi wa barabara,” alisema Jenerali Mabele.
Ameongeza kuwa Suma JKT ni kama wakala wa biashara kati ya Kisiwa cha Ngazidja na Tanzania kwa kufanya biashara ya kusafirisha Ng’ombe na Mbuzi waliohai na mazao kutoka chini kwenda katika visiwa hivyo na kuwa watakuwa na ofisi katika kisiwa hicho ambayo itakuwa inasimamia shughuli zote zinazohusu ushirikiano huo.
“Kwa sasa hivi wamekuja moja kwa moja kwamba wanahitaji mchele ambapo inabidi tushiriki kuhakikisha tunapata mchele Tanzania na tunausafirisha kwenda Comoro,” amesema Jenerali Mabele.
Pia amesema biashara hizo zitakuwa zinazingatia taratibu za nchi zote zinazohitajika na pia itakuwa ni faida kutokana na biashara hizo ni za kimkakati, hivyo itasaidia kuipatia nchi fedha za kigeni kutokana na muingiliano huo wa kibiashara.
Gavana wa Kisiwa cha Ngazidja, Mze Mohamed Ibrahim amesema kinachofanyika ni kuendeleza shirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili ambao umekuwepo na kufanya kazi na Suma JKT itasaidia kuleta ufatiliaji kwa wafanyabiashara wataokao safirisha biashara zao.