Suma JKT yaipiga tafu mama ongea na mwanao

TAASISI ya Mama Ongea na Mwanao ikiongozwa na Steven Mengere ‘Steve Nyerere) imepokea jozi 500 za viatu kutoka Shirika la uzalishaji mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT) ikiwa ni kuunga mkono Kampeni ya “Samia Nivishe Kiatu”
Kampeni hiyo inalenga kuwapatia viatu wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari hususani waishio vijijini
Akizungumza jijini Dar Es Salaam leo Novemba 4,2022 Mkurugenzi Muendeshaji wa kiwanda cha viatu vya ngozi na uzalishaji mali wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Mathias Peter John amesema SUMA JKT inaunga mkono kampeni hiyo ya kizalendo ya kusaidia wanafunzi.
“Hatuwezi kusubiri wachina watuvalishie watoto wetu viatu hivyo tumeamua kwa dhati kuunga mkono jitihada zilizoanzishwa na taasisi hiyo kupitia kwa Mwenyekiti Steven Mengere kuvalisha watoto wa shule za vijijini viatu.”Amesema Meja Mathias na kuongeza
“Tutahakikisha tunatengeneza jozi za kutosha katika kiwanda chetu na kuwapa thamani watoto wetu.” Amesema
Nae, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao, Steven Mengere ametoa shukrani kwa SUMA JKT kwa kuona dhamira ya wazi kuungana nao na kuwasisitiza wasanii kushirikiana na jamii inayowazunguka na kuwathamini kwani ni watu ambao wamekua wakinunua kazi za Sanaa zao.