MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imetoa msaada wa mifuko 200 ya saruji yenye thamani ya Sh milioni tano kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa zahanati na vituo vya afya katika jimbo la Mpanda Vijijini lililopo Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi.
Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya mkurugenzi mkuu, meneja wa kiwanja cha ndege Mpanda, Jeff Shantiwa amesema kufanya hivyo ni utaratibu wao wa kurudisha shukrani kwa jamii kulingana na uhitaji wa eneo husika.
Amesema wametoa mifuko hiyo ya saruji kwa lengo la kushiriki kufanikisha ujenzi wa zahanati pamoja na vituo vya afya vilivyopo jimbo la Mpanda Vijijini.
“Hii sio mara moja, tumekuwa ‘tukisapoti’ ujenzi wa madarasa, zahanati na miradi mbalimbali ya maendeleo” amesema Shantiwa.
Akizungumza kwa niaba ya Mbunge wa jimbo la Mpanda Vijijini, katibu wa mbunge huyo, Said Wambali ameishukuru TAA kwa kusaidia kufanikisha ujenzi wa Vituo vya Afya na Zahanati huku akisema miradi hiyo itakapokamilika itasaidia kutatua changamoto za miradi iliyokwama katika jimbo hilo.
SOMA: Wapewa msaada ujenzi wa shule Inyagantambo
“Katika maeneo mbalimbali ya Kata na vijiji ndani ya jimbo hili, miradi hii imekuwa ikikwama kwa sababu ya kukosa vifaa vya ujenzi kama simenti, mabati nakadhalika” amesema Wambali.