Taasisi 369 za serikali zatumia nishati safi
TAASISI za serikali zipatazo 369 zimeunga mkono agizo la Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira kwa kuacha kutumia nishati ya kuni na mkaa na badala yake kuingia katika matumizi ya nishati safi na salama.
Meneja wa mauzo kwa wateja wa Taifa Gas Tanzania Limited, Moses Massawe alisema hayo juzi wakati wa utoaji mafunzo kwa waandishi wa habari wa Mkoa wa Morogoro kuhusu kampeni ya utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati safi na salama, tukomeshe uvunaji wa miti kiholela.
Massawe alisema Taifa Gas inaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika suala la uhifadhi na utunzaji wa mazingira, hivyo imeweka mkakati wa utoaji wa elimu juu ya madhara ya matumizi ya kuni na mkaa.
“Hadi sasa tumezifikia taasisi 369 za umma ambazo zinatumia nishati safi na salama na katika Mkoa wa Morogoro zipo taasisi nane zimeunganishwa na matumizi haya na hivyo zimeondokana na kutumia kuni na mkaa,” alisema.
Massawe alisema katika kukabiliana na changamoto hizo, Taifa Gas kuanzia Julai hadi Desemba mwaka huu imeweka mkakati kuzifikia taasisi 460 na hivyo kufanya jumla ya taasisi 829.
Naye Mkuu wa Chuo cha Ualimu Morogoro, Augustine Sahili ambaye chuo chake kimeachana na matumizi ya kuni na mkaa baada ya kuunganishiwa gesi alisema tangu kuanza kutumia nishati hiyo wameweza kuokoa Sh milioni 15 kwa mwaka.
Mei 18, 2018 serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais iliagiza taasisi za serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali na mengine yenye matumizi makubwa ya kuni na mkaa, yatumie nishati mbadala kwa kupikia ikiwa ni njia mojawapo ya kupunguza uharibifu wa mazingira.