TAASISI ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) imesaini mkataba wa makubaliano ya ujuzi wa kidijiti na Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia mafunzo ya Kompyuta(ICDL) kwa lengo la kuongeza ufanisi katika ufundishaji.
Makamu Mkuu wa NM-AIST, Profesa Emmanuel Luoga alisema Nelson Mandela imeamua kushirikiana na ICDL Afrika ili kuleta umahiri na ufanisi wa kazi, kujenga uwezo wa kidijiti katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo na kielimu katika kukuza sekta ya mawasiliano nchini .
“Tunataka taasisi yetu iwe ya kwanza katika umahiri wa utoaji ujuzi wa kidijiti katika masuala ya kompyuta,” alisema.
Naye Meneja wa Kanda wa ICDL nchini, Edwin Masanta alisema wameamua kushirikiana na Taasisi ya Nelson Mandela katika kuhakikisha wanaongeza utendaji kazi na ufanisi.
Aidha, alisema Tanzania ya viwanda ni lazima iweze kuendana na kasi ya teknolojia ya kompyuta katika kuhakikisha ubora wa maendeleo unaendana na kasi ya ukuaji wa uchumi kwa kutumia kompyuta.
Kwa upande wake Mhadhiri kutoka Taasisi ya Nelson Mandela kwa niaba ya Kaimu Naibu Makamu Mkuu, Mipango, Teknolojia na Utawala, Profesa Kelvin Mtei alisema programu hiyo ya kompyuta itaongeza tija ya ufanisi katika utendaji kazi katika kukuza uchumi.