Taasisi yafadhili mafunzo ufugaji nyuki

Taasisi ya LALJI FOUNDATION kwa kushrikikiana na Chama Cha Wanawake Wajane Tanzania (CCWWT) kimefadhili mafunzo ya ufugaji nyuki na utengenezaji wa mizinga kwa wanawake mjini Bagamoyo ambapo Wakina mama zaidi ya 100 kutoka mikoa 10 walishiriki kwenye mafunzo hayo.

Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo wanawake na vikundi vya kijamii maarifa ya kisasa ya ufugaji nyuki, utunzaji wa mizinga, uvunaji salama wa asali pamoja na mbinu bora za kuongeza thamani ya mazao ya nyuki.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Mratibu wa Miradi kutoka LALJI FOUNDATION, Judith Kahatano, alieleza kuwa lengo kuu la mpango huo ni kuwawezesha wanawake kujitegemea kiuchumi kupitia miradi endelevu inayoweza kuongeza kipato cha familia na kuchangia maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Alisisitiza kuwa taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha mafunzo hayo hayabaki kuwa ya muda mfupi, bali yanazaa matokeo ya kudumu katika jamii.

Kwa upande wake Mkufunzi wa Ufugaji Nyuki kutoka Tanzania Forest Services Agency (TFS), Vincent Mnaya, amesema ufugaji wa nyuki ni biashara yenye tija kubwa kiuchumi na kimazingira, na amewahimiza wanufaika kuzingatia mafunzo na usimamizi sahihi ili kupata matokeo chanya.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Wanawake Wajane Tanzania (CCWWT), Rabia Moyo, ameishukuru LALJI FOUNDATION kwa mafunzo ayo akieleza kuwa yatasaidia kuongeza kipato kwa wajane na kuboresha ustawi wa familia zao kupitia ufugaji nyuki.

Wanufaika wa mafunzo hayo walitoa shukrani kwa ufadhili huo, wakisema kuwa maarifa waliyopata yatawasaidia kuanzisha au kuboresha miradi yao ya ufugaji nyuki na hivyo kuboresha hali zao za maisha.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button