Taasisi yatoa mil 150/- kuinua vijana Arusha

ARUSHA: TAASISI ya Nasimama na Mama Tanzania (TNMT) imetenga zaidi ya Sh milioni 150 kwa ajili ya kuwainuwa kiuchumi vijana na wanawake waliopo katika kata 15 za jiji la Arusha.
Hayo yalisemwa leo jijini Arusha na Mwenyekiti wa TNMT Kanda ya Kaskazini, Monica Suleiman mbele ya waandishi wa habari na kusema kuwa kila kata itapewa shilingi milioni 10 na kila kikundi kinatakiwa kuwa na vijana ama wanawake wasiozidi kumi watakaotambulika na viongozi wa serikali ngazi ya kata .
Suleiman alisema kuwa TNMT imejipanga kuhakikisha inawakomboa vijana na wanawake kujikwamua kiuchumi kwa kuwapa mtaji wa kuanzisha miradi ya maendeleo kama mradi wa ufugaji na kilimo na kuacha kutegemea ajira serikali ambazo ni finyu.

Mwenyekiti huyo aliendelea kusema kuwa kabla ya kutoa fedha kwa vikundi hivyo watawawezesha vijana na wanawake kupata elimu ya mradi ili watakapoanzisha mradi wawe na uelewa mpana ikiwa ni njia mojawapo ya kutaa mradi huo uwe endelevu na sio vinginevyo.
Sulemani alisema mbali ya kutoa fedha kwa vijana na wanawake katika kuanzisha miradi pia TNMT inajikita katika kuisemea serikali jinsi inavyofanya vizuri katika kuanzisha miradi midogo na mikubwa kwa ajili ya maendeleo ya nchi kwa kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Alisema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akifanya mambo mengi makubwa ikiwemo miradi ya maendeleo lakini kuna baadhi ya watu wamekuwa wakibeza jitihada hizo hivyo TNMT imekuja kivingine kuhakikisha miradi yote iliyomjaliziwa na inayobuniwa na Rais inaelezewa kisawasawa na taasisi ili kila mwananchi wa mjini na kijiji kujua hilo.
Aidha Mwenyekiti wa TNMT alisema kuwa taasisi hiyo inajikita katika kushawishi wanawake mjini na kijiji kujitokeza kwa wingi katika kuwania nafasi mbalimbali za uongozi na wameweza kufanikiwa katika wilaya ya Longido na Ngorongoro kwani wanawake wamechukua fomu kuwania udiwani na wamefanikiwa kupita bila kupingwa.

Mwenyekiti alisema katika miaka ijayo ya uchaguzi ana uhakika muitikio kwa wanawake utakuwa mkubwa kwani wengi wao wameonyesha kujitoa na kuondoa woga katika kuwania nafasi ya uongozi katika chaguzi.
Naye Afisa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA),Iddy Kaluse aliipongeza TNMT kwa kuja na mpango huo wenye tija kwa nchi na kusema kuwa Shirika la litaunga mkono jitihada hizo ikiwa ni njia mojawapo ya kuhamashisha utalii wa ndani na kuongeza mapato ya nchi.
Kasule alisema taasisi hiyo ikitangaza zaidi utalii wa ndani katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ana uhakika wa ongezeko la watalii wa ndani ikiwa ni njia mojawapo ya kuunga mkono jitihada za Rais katika filamu yake ya The Royal Tour.
Katibu wa TNMT Kanda ya kaskazini,Dionis Moyo alisema kuwa taasisi hiyo sepetemba 30 mwaka itafanya maandamano ya amani yenye lengo la kuhamashisha amani na utulivu wakati wa uchaguzi Mkuu octoba 29 mwaka huu na baada ya uchaguzi ili wananchi waweze kuchaguzi wagombea wanaowataka kuwaongoza hapa nchini.
Moyo alisema msafgara wa maandamano utaanzia mnara wa saa na kuishia viwanja vya Makumbusho ya Azimio la Arusha na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa wilaya ya Arusha Joseph Mkude.



