DAR ES SALAAM; IMEKUWAJE Tabora United kuifunga Yanga?Ni swali wanalojiuliza mashabiki wa mpira wa miguu na hasa wadau wa Yanga.
Hakika ni matokeo ambayo hayakutarajiwa na wengi, lakini ndivyo soka lilivyo, Yanga imekubali kipigo cha mabao 3-1 nyumbani, mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baina ya timu hizo uliomalizika muda mfupi uliopita Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam.
Tabora United ilienda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0, mfungaji akiwa Offen Chikola, huku mashabiki wakishuhudia Aziz Ki akipoteza mkwaju wa penalti kwa Yanga uliodakwa na kipa Hussein Masalanga.
Bao la tatu la Tabora lilifungwa dakika ya 78 mfungaji akiwa Ibrahim Ahmada, wakati bao la kufutia machozi la Yanga likifungwa na Clement Mzize dakika za jioni kabisa.
Kwa matokeo hayo Tabora United sasa imepanda hadi nafasi ya sita baada ya kufikisha pointi 17, huku Yanga ikisalia nafasi ya pili ikiwa na pointi 14 nyuma ya vinara Simba wanaoongoza wakiwa na pointi 25.