BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Kanda ya Kusini imetoa mafunzo kwa viongozi zaidi ya 100 kutoka vyama mbalimbali vya msingi katika Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara kuhusu elimu ya matumizi sahihi ya usimamizi wa fedha.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani humo, Meneja wa Benki hiyo Kanda ya Kusini, Zaidi Ramadhani amesema katika wilaya hiyo wanatarajia kuwa na idadi hiyo ya viongozi waliopata mafunzo hayo kwa mwaka 2024.
Mafunzo hayo yanalengo kuwajengea uwelewa zaidi katika suala hilo la matumizi sahihi ya usimamizi wa fedha pia namna mzuri ya kutenga bajeti ya uendelezaji katika fedha za mkopo na kuleta tija kwa Amcos zao pamoja na wakulima wanaowahudumia.
Aidha, moja ya mada iliyotolewa katika mafunzo hayo ikiwemo nidhamu ya fedha, namna ya kuwandaa bajeti, kuwandaa matumizi ya fedha kabla ya kuanza matumizi yoyote, wanapotaka kufanya uwekezaji waanze na uchunguzi wa eneo au kile wanachotaka kukifanya kabla ya kuanza kazi hiyo na mengine.
‘’Mafunzo hayo yawasaidie nyinyi katika kuibua miradi na yafike kwa wengine waliyoko chini yenu, mnavopata mafunzo muwe na uwezo wa kutathamini kwenye vyama vyenu, kwamba hivi chama changu kina mahitaji yoyote ya mkopo na kuna namna yoyote ile tunaweza kuanzisha miradi na tukapata mikopo, ’’amesema Zaidi.
Kaimu Mrajisi mkoani humo, Mohamedi Lilanga amesema mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo wanayopatiwa katika vyama vyao hivyo watambue kuwa nyuma yao kuna watu wengi wanaowategemea hasa kuhusu elimu hiyo wanayopatiwa na benki hiyo.
SOMA: Majaliwa azindua benki ya TADB Kanda ya Kusini
‘’Dozi hii leo isiwe tu kwenu ishushwe chini kwa wakulima kama tunavyofahamu Tadb ni taasisi ya serikali inayodili na mambo ya kilimo na sisi kama viongozi tunaosimamia wengi asilimia kubwa ni wakulima tuwape hii dozi lakini elimu hii na waliyoko chini yetu wapate manufaa ya hii taasisi ya seriali,’’amesema Lilanga.
Katibu Mkuu wa Chama cha Misingi cha Namayanga Amcos katika Manispaa ya Mtwara Mikindani, Mwanahawa Ahmad amesema:‘’Mafunzo yanatija kubwa kwangu kwasababu kuna baadhi ya vitu nimevitambua leo ambayo nilikuwa sivifahamu awali hasa upande wa nidhamu ya fedha’’
Mwenyekiti wa Chama cha Misingi cha Mtwara Amcos kwenye manipaa hiyo, Ismail Ally amesema elimu hiyo itamsaidia kufahamu jinsi ya kutenga bajeti ya uendelezaji katika fedha ya mkopo na marejesho kwa ujumla pia uwepo wa benki hiyo ni ukombozi mkubwa kwa wakulima na Amcos wilayani humo hasa katika suala la mikopo.