Takukuru yaonya wazabuni wasiofuata utaratibu Geita

GEITA; Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Geita, imewataka wazabuni wanaopewa kazi ya kusambaza vifaa ujenzi katika miradi tofauti kuhakikisha wanazingatia Makadirio Halisi ya Gharama za Ujenzi (BoQ).
Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Geita, Alex Mpemba ametoa maagizo hayo wakati akiwasilisha taarifa ya taasisi kwa waandishi wa habari na kueleza hawatosita kuchukua hatua kwa yeyote atakayehujumu miradi.
Mpemba amesema uchunguzi wa TAKUKURU kipindi cha mwezi Aprili hadi Septemba 2026, umebaini kuwa miradi 32 kati ya 38 katika sekta ya elimu, afya, barabara, maji na miradi ya maendeleo ya jamii ilikutwa na mapungufu.
Amesema uchunguzi huo ulifanikisha fedha kiasi cha Sh milioni 24.6 kurejeshwa kutokana na matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi 38 yenye thamani ya Sh milioni 61.5 baada ya kubaini changamoto katika miradi hiyo.

Mpemba amesema TAKUKURU pia ilibaini kasoro kubwa katika miradi sita na kudhibiti malipo ya sh milioni 2.4 yasilipwe kwa mzabuni baada ya kuwasilisha madawati 30 yaliyokuwa yametengenezwa kwa mabo mbichi.
Amesema mkandarasi huyo alifanya kazi hiyo kinyume na mashariti ya mkataba katika ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya msingi Butambala iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Bukombe mkoani humo.
Amesema pia TAKUKURU imedhibiti malipo ya Sh milioni 10.3 yasilipwe kwa mzabuni aliyetengeneza milango 24 iliyo chini ya kiwango na kinyume na BOQ katika jengo la OPD Kituo cha Afya Busolwa wilayani Nyang’hwale.
“Katika kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026 jumla ya Shilingi milioni 242 zimedhibitiwa na kuokolewa kupitia ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za utetekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Wazabuni wote wanapaswa wafuate BOQ kwa sababu BOQ ndio mkataba wa kazi, maana yake unapoenda kinyume na BOQ ni hujuma”, amesema Mpemba.



