TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Mtwara imesaidia kufanya miradi minane kujengwa kwenye ubora unaotakiwa mkoani humo.
Akizungumza jana mkoani humo, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mtwara Mashauri, Elisante amesema kuanzia Oktoba hadi Desemba 2024 wamefanikiwa kukagua miradi 28 yenye thamani ya Sh milioni 10.9 katika sekta ya elimu na miundombinu ya afya.
Ameongeza kuwa kati ya miradi hiyo miradi yenye thamani ya Sh milioni 253.3 ilikutwa na mapungufu madogo madogo ambapo walitoa ushauri na mapendekezo katika miradi hiyo 8 na kufanikiwa kujengwa kwenye ubora uliyokusudiwa.
Aidha miradi hiyo ni pamoja na mradi wa ujenzi wa matundu manne ya vyoo katika shule ya msingi Makonga iliyopo halmashauri ya Wilaya Newala wenye thamani ya Sh milioni 6.8 ambapo fedha za utekelezaji ziliisha kabla ya milango kufungwa.
Aidha kufuatia hilo, takukuru ilitoa maazimio ya kuwa ofisi ya mkurugenzi kutumia fedha za mapato ya ndani kukamilisha kazi zilizobaki kwa muda wa wiki mbili na hadi sasa utekelezaji umefanyika.
Katika sekta ya afya, daktari wa zahanati ya Mnolela Kata ya Malatu iliyopo Wilaya ya Newala kutoa huduma mbovu kwa wagonjwa na taasisi hiyo imefanikiwa kutatua kero hiyo kwani daktari huyo alipewa barua ya onyo pamoja na kuhamishwa kituo.
Aidha, sekta ya ardhi taasisi hiyo imemtaka mtendaji wa kijiji cha malatu shuleni wilayani humo, Hamisi Chilumba kutojihusisha na majukumu ya kutatua migogoro ya ardhi kutokana na wananchi wa kata hiyo kumlalamikia mtendaji huyo kwa kuwanyanyasa na kuwaomba fedha wanapoenda kutatua migogoro hiyo.
Pia mradi wa ujenzi wa jengo moja la darasa shule ya sekondari chawi iliyopo Halmashauri ya Mji Nanyamba wenye thamani ya Sh milioni 24 ambapo hadi kufikia siku ya ukaguzi Oktoba 30,2024 mlango kwenye jengo hilo haukuwa umekamilika hali ya kuwa malipo yalikuwa yameshafanyika hivyo mzabuni alitakiwa kukamilisha kazi hiyo kabla ya Novemba 08,2024 na hadi sasa mlango umefungwa.