Takukuru yazuia magari ya Kigoma kutoa huduma

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imefanikiwa kutoa suluhisho la kero ya muda mrefu ya mabasi mabovu ya kampuni ya Kigoma yaliyokuwa yanatoa huduma kati ya Iringa Mjini na kata ya Malengamakali Iringa vijijini.

Ubovu wa mabasi hayo umeelezwa na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Iringa, Domina Mukama kwamba ulikuwa unahatarisha maisha ya wananchi waliokuwa wakiyatumia kwasababu ya kuharibika mara kwa mara yawapo safarini.

Pamoja na kuharibika Mukama alisema wahusika wa mabasi hayo walikuwa na kawaida ya kutorudisha nauli kwa abiria na kukataa kuwabadilishia magari mengine ili wamalizie safari zao.

Advertisement

“Baada ya Takukuru kupokea kero hiyo katika kikao cha kuibua kero cha Takukuru Rafiki kilichofanyika katani hapo, tuliwakutanisha viongozi wa polisi na Latra na kuchukua hatua za kusimamisha magari hayo kutoa huduma,” alisema.

Alisema mmiliki wa mabasi hayo amepewa sharti la kuyafanyia matengenezo makubwa na atakapokamilisha ukaguzi utafanywa na yatakapobainika yapo sawa yatabadilishiwa njia.

“Hayatarudi njia ile ile kwani wananchi hawana imani tena ya kuendelea kupewa huduma hiyo kupitia mabasi hayo,” alisema.

Aidha alisema katika utekelezaji wa huduma hiyo ya Takukuru Rafiki wameweza kuzifikia kata tisa katika kipindi cha Julai hadi Septemba huku kero mbalimbali katika sekta ya polisi, maji, afya, elimu, barabara, nishati na kilimo zikiibuliwa na kupatiwa ufumbuzi.

“Lakini pia kwa kupitia programu hiyo tumeokoa kiasi cha Sh milioni 2.4 zilizokuwa zimedhulumiwa na baadhi ya viongozi wa kikundi cha vikoba cha Bumilayinga Saccos Mafinga kilichovunjwa Disemba 2022,” alisema.

Kwa upande wa ufuatiliaji wa rasilimali za umma alisema katika kipindi hicho cha Julai hadi Septemba Takukuru imefuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo 18 yenye thamani ya Sh bilioni 3 katika sekta za ujenzi, elimu na afya.

Kati ya miradi hiyo Mukama alisema mitatu ilionekana kuwa na mapungufu na hatua mbalimbali zimechukuliwa kurekebisha.

Aidha alisema wamepokea malalamiko 41 yakiwemo 29 ya rushwa yaliyoshughulikiwa kwa mujibu wa sheria kwa kuanzisha uchunguzi uliofikia hatua mbalimbali.

3 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *