Tamasha la Busara kukusanya mamilioni ya fedha

TAMASHA la Kimataifa la Sauti za Busara msimu wa 2025 linatarajia kutengeneza dola milioni 10 za mapato kwa uchumi wa ndani wa Zanzibar.

Akizungumza Dar es Salaam kuhusu ujio wa tamasha hilo la siku tatu litakalofanyika Zanzibar kuanzia Februari 14 hadi 16, Mkurugenzi Mtendaji wa Busara Promotion Lorenz Herrmann amesema matokeo hayo ndio wanayoyatarajia kuyapata kwenye tamasha hilo.

“Tunatarajia kutengeneza fedha na kuongeza mapato ya ndani ya Zanzibar kutokana na wageni wengi na watalii watakaokuja kwenye tamasha letu, hayo ni miongoni mwa matokeo ya kiuchumi tunayotarajia,”amesema.

Advertisement

Amesema pia, tamasha hilo linatarajia kutengeneza fursa za ajira 200 zitakazowanufaisha watu wa Zanzibar.Herman amewashukuru wadau mbalimbali waliosapoti tamasha hilo akisema wanajivunia kuwa na wadau 45.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa tamasha Journey Ramadhan amesema Limekutanisha wasanii kutoka sehemu mbalimbali wakiwemo Frida Amani, Bendi ya Malaika chini ya Christian Bella, Blinky Billy kutoka Kenya na wengine kutoka Afrika Kusini, Zanzibar, Rwanda, Tunisia, Sudan na kwingineko duniani.

Amesema pia, kutakuwa na makongamano yatakayowakutanisha wadau mbalimbali wa muziki kuzungumzia changamoto wanazopitia wanazopitia katika tasnia ya muziki.

“Kauli mbiu yetu ni Amani ndio mpango mzima, tunaamini kupitia muziki utakuwa ni silaha tosha ya kupeleka ujumbe wa kutuliza hali ya kifarakano ambayo dunia inaiona sehemu mbalimbali duniani,”amesema.

Mwenyekiti wa Bodi wa Sauti za Busara Simai Said Mohamed amesema ujio wa tamasha hilo ni bahati kwa Wazanzibar na kwa Watanzania na kuwahimiza waendelee kuwa wakarimu kwa wageni watakaokuja.

“Tanzania tunaenda kuzungumzwa kwa uzuri wetu, utamaduni wetu na katika kujenga fursa za uchumi. Sauti za busara kuna mambo mengi ndani yake kutakuwa na kazi ya kuwaunganisha watanzania,”amesema.

Balozi wa Umoja wa Ulaya Christine Grau amesema mwaka huu watashiriki katika jukwaa la wanawake na anathamini serikali ya Zanzibar katika kukuza juhudi za usawa wa kijinsia.

Amesema anategemea mambo mbalimbali yatajadiliwa ikiwemo program za jinsia katika kampeni, uwezeshaji wa wanawake kiuchumi na kiuongozi namna ya kuondokana na unyanyaji na kuelezea majukumu ya mwanamke katika muziki.